TRA Geita yakusanya bil 34/ miezi sita

MAMLAKA ya Mapato (TRA) Mkoa wa Geita imekusanya kiasi cha sh bilioni 34.44 sawa na asilimia 109.76 ya lengo la kukusanya sh bilioni 30.47 kwa miezi sita ya mwaka wa fedha 2024/25.

Kamishina wa Kodi za Ndani kutoka TRA, Alfred Mregi amesema hayo katika hafla ya kuadhimisha kilele cha wiki ya mlipa kodi kwa mkoa wa Geita kwa mwaka wa fedha wa 2023/24.

Amesema hatua hiyo ni kiashiria cha mafanikio ya sera ya serikali ya awamu ya sita inayoelekeza mahusiano mazuri kati ya TRA na walipa kodi ili kuchagiza ulipa kodi wa hiari pasipo kuwa na migogoro yeyote.

Amesema kwa upande wa Mamlaka ya Mapato kwa Ujumla wake kitaifa iliweka lengo la kukusanya sh trillioni 15.8, na mpaka sasa imeweza kukusanya kiasi cha sh trillion 16.5 ndani ya kipindi cha miezi sita.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa bajeti yetu ya serikali TRA inatarajia kukusanya sh trilioni 30.4, kwa mkoa wa Geita tunatarajia kukusanya sh bilioni 61.7″, amesema Mregi

Amesema miongozo na maagizo mbalimbali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan imekuwa nguzo muhimu katika usimamizi wa kodi hatimaye kuongezeka kwa tija na ufanisi katika ukusanyaji wa kodi.

“Serikali inaheshimu mchango wa kila mlipakodi, katika taifa hili bila kujali ukubwa wa kodi anayolipa, au udogo wa kodi anayolipa kwa sababu kila mtu analipa kulingana na uwezo wake”, amesema.

Amesema mbali na mafanikio yaliyopo bado kuna changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kuendekeza matumizi yasiyo sahihi ya Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD).

“Suala la ukwepaji kodi kwa matumizi yaiyo sahihi ya EFD, ni suala pana na mtambuka na linawagusa wanunuzi na wafanyabiashara kwa pamoja, hivo ni suala linalohitaji ushirikiano”, amesema.

Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amewaomba wafanyabiashara kutambua, kodi ipo kwa mjibu wa sheria na serikali haipo tayari kumuonea wala kumpendelea mtu katika kutekeleza sheria hiyo.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara (TCCIA) Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel ameomba serikali kuendelea kutengeneza mazingira rafiki ya mikopo yenye mashariti nafuu kwa wafanyabiashara ili kupanua uwigo wa uwekezaji.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba alisisitiza wafanyabiashara kuheshimu sheri na kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuondoa mivutano isiyo ya lazima kati yao na TRA.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button