TRA Kagera kuwezesha wafanyabiashara

KAGERA: Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera imezindua Dawati Maalumu la Uwezeshaji Biashara kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo ili kuendelea kuweka mazingira bora ya kufanya biashara.
Akizindua huduma hiyo katika ofisi za mkoa za TRA, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa aliushukuru uongozi wa mamlaka hiyo kwa ubunifu na kuanzisha huduma ya kuweka mazingira rafiki ili wafanyabiashara wafanye shughuli zao kwa uhuru zaidi huku wakilipa mapato ya Serikali bila usumbufu.
“TRA ya sasa ni rafiki sana, si kama ya zamani, unakaribishwa, unaelekezwa unakadiriwa kulingana na biashara yako, unapewa muda wakulipa kodi kidogo kidogo kama umelimbikiza kodi lakini pia kama kuna jambo hulielewi unaelimishwa,” amesema Mwassa
Mkuu huyo wa mkoa alitoa pendekezo kwa TRA kuanzisha huduma ya ‘club shuleni’ kwa watoto inayohusu ulipaji kodi ili watoto wakue wakijua umuhimu wa kodi kwa baadhi hawajui kuwa kadri unavyokataa kulipa kodi ndivyo unavyochelewesha maendeleo.
Aidha alisema huenda dirisha Hilo maalumu likawa msaada kwa wafanyabiashara wengi Wa mji wa Bukoba wanaopanga bidhaa chini wakiamini kuwa mfanyabiashara mdogo hapaswi kuwa na eneo zuri la kufanyia biashara huku akidai kuwa wapi wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa waliojificha katika kivuli Cha kumwaga bidhaa zao chini
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa aliwakumbusha TRA mkoa wa Kagera kuhakikisha wanawafikia walipa kodi wote ili kukusanya mapato ya Serikali hususani kwa wafugaji ambao wanamiliki ng’ombe wengi katika ranchi za mkoa wa Kagera ampabo amewahaidi TRA kuwakutanusha na wafugaji hao
Aliwataka wafanyabiashara kutumia fursa ya dawati maalum la uwezeshaji biashara kupata ushauri ili kukuza zaidi biashara zao na kudai kuwa kufanya biashara katika mazingira ya chini sio sifa nzuri na badala yake wafanyabiashara wanapaswa kubadilika
Husna Abdul Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga mkoa wa Kagera akiongea katika uzinduzi huo aliushukuru uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kagera kwa kuwa karibu na wafanyabiashara wadogo hususani wamachinga kwa kuwapokea na kuwaelimisha huku wakiwaongoza ili nao wakuze mitaji yao na biashara zao pia.
Castro John Meneja wa Mamlaka ya Mapatoa Tanzania TRA Mkoa wa Kagera amesema huduma ya Dawati la Uwezeshaji Biashara imefunguliwa na kuzinduliwa rasmi katika Mkoa wa Kagera lengo kuu likiwa ni kuwatambua, kuwasikiliza na kuwawezesha wafanyabiashara wakiwemo wale wadogo kabisa kukuza biashara zao na kulipa mapato ya Serikali.
Alisema madawati hayo pia yapo katika halmashauri zote za mkoa wa Kagera kwenye ofisi za TRA hivyo wafanya biashara watakaohitaji kuunganishwa na taasisi zinazotoa Mikopo na mitaji kwa riba nafuu wataunganishwa haraka bila changamoto .



