Treni 5 SGR kubeba mizigo bandarini Dar kwa siku

SERIKALI imetaja mikakati ya kupunguza msongamano wa makasha ndani ya Bandari ya Dar es Salaam ikiwemo kuongeza safari za Treni ya Kisasa (SGR) ya mizigo.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema kuanzia Febuari 15, serikali itaongeza treni tano za mizigo kusafirisha makasha kupeleka bandari ya Kwala mkoani Pwani na Ihumwa, Dodoma.

Profesa Mbarawa alieleza hayo alipotembelea na kukagua bandari hiyo na kuona msongamano wa makasha uliotokana na kuongezeka kwa ufanisi wa bandari katika kushusha mizigo baada ya uwekezaji wa DP World na kampuni ya Tanzania East Africa Gateway Terminal.

Profesa Mbarawa alisema kwa sasa bandari hiyo inapokea treni moja ya mizigo inayoweza kubeba makasha 200, hivyo ongezeko la treni tano kutasaidia kupunguza msongamano.

SOMA: Mizigo SGR neema kwa nchi

“Bandari ya Dar es Salaam kwa siku ilikua inakuja treni moja ambayo ilikua inachukua makontena (makasha) 200 sasa tumekubaliana itakapofika kuanzia Februari 15, tutaongeza treni tano na bado tuna treni nyingine tano tuna treni 10 zinazoweza kutoa huduma, haya yote tunafanya ili bandari yetu iweze kupumua,” alisema.

Aidha, Profesa Mbarawa alisema uwekezaji wa bandari pia umeongeza mapato ya bandari kutoka Sh bilioni 700 kwa mwaka mpaka Sh trilioni 2.03 kwa sasa.

Sambamba na kuongeza safari za treni ya mizigo, serikali imesema Kampuni ya East Africa Gateways Terminal inaendelea na ujenzi wa Bandari kavu ya Kurasini itakayosaidia pia kupunguza msongamano katika bandari ya Dar es Salaam.

Ujenzi wa bandari hiyo ya Kurasini umefikia asilimia 90 na unatarajia kukamilika mwishoni mwa Februari huku kipande cha kwanza kitakua na uwezo wa kuhifadhi makasha 150,000.

Profesa Mbarawa alisema uwekezaji wa kampuni hizo binafsi umeongeza idadi ya makasha yanayohudumiwa kutoka 800,000 mwaka 2020 hadi 1,300,000 mwaka 2025 ongezeko la asilimia 50 na matarajio ni kufikia makasha milioni mbili.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abeid Gallus alisema ufanisi wa wawekezaji umewezesha kupunguza muda wa kushusha mizigo kutoka siku saba mpaka siku tatu huku wastani wa meli kusubiri nangani umepungua hadi siku tano.

Mkuu wa wa Uhusiano na Uratibu wa Shughuli za Kampuni kutoka DP World, Elitunu Mallamia alisema hadi
kufikia Januari 2026 kampuni hiyo imehudumia makasha kwa asilimia 68 kulinganisha na kipindi kama hicho 2025
huku kwa Desemba 2025 kampuni hiyo ilihudumia makasha kwa asilimia 94 kulinganisha Desemba 2024 ikionesha kuna ongezeko la makasha yanayohudumiwa na kampuni hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button