TSN, VIORY kushirikiana kukabili upotoshaji taarifa

KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) imekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Mtandao wa Habari wa Viory Video Network wa Abu Dhabi, Dubai, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kupambana na upotoshaji wa taarifa, hususan katika majukwaa ya kidijitali.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo, Februari 10, 2026, katika Ofisi Kuu za TSN zilizopo jijini Dar es Salaam, ambapo katika kikao hicho, pande zote mbili zimekubaliana kushirikiana katika kubadilishana maudhui ya msingi ya uzalishaji wa habari na video za habari zilizohakikiwa, kuanzisha miradi ya pamoja katika uandishi wa habari za kidijitali, pamoja na kutekeleza programu za kujenga uwezo zitakazoimarisha ujuzi wa uzalishaji wa video, uhakiki wa taarifa na uandishi wa habari unaozingatia maadili ya taaluma.

Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi, amesema kuwa pamoja na makubaliano hayo, pande hizo pia zimekubaliana kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, hususan katika utendaji wa kazi ndani ya tasnia ya habari.

“Tumekutana kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujadili namna bora ya kupambana na upotoshaji wa taarifa kwa lengo la kuimarisha maudhui ya kidijitali. Hii ni fursa muhimu kwa TSN, kwani tumeweza kukubaliana misingi ya kushughulikia upotoshaji ambao mara nyingi unatolewa kutoka nje ya nchi. Kupitia ushirikiano huu, tutapata nafasi ya kusimulia habari zetu kwa mtazamo wa Kitanzania na hivyo kuijenga nchi yetu,” amesema Dachi.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo hautaimarisha tu maudhui ya TSN, bali pia utaongeza uwezo wa taasisi katika kuwasilisha simulizi zenye athari kuhusu maendeleo kwa hadhira ya ndani, kikanda na kimataifa.

“Tuko tayari kushirikiana katika ubunifu wa kidijitali, usambazaji wa maudhui na matumizi bora ya majukwaa ya mtandaoni, mradi juhudi hizo ziendane na dhamira yetu ya kutoa huduma kwa umma na kuheshimu kikamilifu uhuru wetu wa uhariri,” amesisitiza.

Dachi amebainisha kwamba kupitia ushirikiano huo, TSN itanufaika kwa kupata uzoefu wa kimataifa kutoka Viory, hususan katika matumizi ya mbinu bora za kimataifa, mifumo ya mawasiliano iliyoandaliwa vizuri, pamoja na uandishi wa habari unaojikita katika maendeleo, uwekezaji na ubunifu.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Afrika wa Viory Video Network, Alexander Kobia, amesema lengo kuu la ziara yao ni kutafuta ushirikiano kama mtandao wa kimataifa wa video za habari pamoja na kubadilishana maudhui ili kuhakikisha habari za Tanzania zinaifikia dunia kwa upana.

“Tunataka habari za Tanzania zisikike duniani kwa namna ileile ambayo habari za mataifa mengine yenye mwelekeo sawa zinavyosimuliwa hapa Tanzania. Viory inaweka mkazo katika nchi za Kusini mwa Dunia, ikiwemo mataifa ya BRICS, na tunalenga kuzifikisha habari hizo kwa hadhira ya kimataifa,” amesema Kobia.

Ameongeza kuwa kipaumbele cha Viory ni kuangazia habari chanya ambazo mara nyingi hazipewi nafasi kubwa katika vyombo vya habari, akibainisha kuwa ndiyo sababu mtandao huo hujieleza kama sauti ya wasiokuwa na sauti.

Kobia pia amesema kuwa ushirikiano huo utajumuisha matumizi ya teknolojia mpya, hususan akili bandia (AI), katika uzalishaji na uhakiki wa maudhui, pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi bora ya mitandao ya kijamii na mbinu za kisasa za uwasilishaji wa habari.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button