Tuchukue tahadhari madhara ya mvua

TANGU zilipoanza mvua zinazoendelea katika maeneo mengi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kumekuwa na taarifa mbalimbali kuhusu madhara yatokanayo na mvua hizo.
Kwa kiasi kikubwa, madhara hayo ya mafuriko ni matokeo ya athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na mambo mbalimbali ukiwamo uharibifu wa mazingira.
Miongoni mwa madhara ya mvua hizo ni vifo vya mamia kwa makumi ya watu, majeruhi, uharibifu wa mali na watu kuyakimbia makazi.
Sisi tunatoa pole kwa nchi zote za EAC ambazo watu wake wamefikwa na madhara haya ama kwa kuharibikiwa na kupoteza mali, kujeruhiwa au ndugu zao kupoteza maisha.
Hata hivyo, wakati tukiungana na wote wenye mapenzi mema kuwaombea faraja ndugu hao katika nchi zote, tunasisitiza wananchi wote popote walipo kuchukua tahadhari dhidi ya matishio yote ama ya mafuriko ya maji au maporomoko ya udongo.
Tunasema, waishio katika mabonde na mikondo ya maji, wasisubiri kuambiwa ‘pole’ au kuonewa huruma, bali wawe walinzi wa kwanza wa nafsi na familia zao kwa kutoka katika maeneo yote hatarishi.
Aidha, tunawashauri waishio kando ya milima katika nchi hizo na kwingineko barani Afrika, wazinduke mapema ili kukwepa hatari ya kutokea ama maporomoko ya udongo au mawe yanayosababisha madhara makubwa kwa jamii.
Tahadhari nyingine ni watu kuepuka ‘kupima kina cha maji kwa miguu’ hasa madereva wenye kasumba ya kudharau mafuriko ya maji yanayovunja kingo za barabara na madaraja na kusambaa.
Hawa ni wale wanaoyapuuza na kuamua kuyavuka bila kujua hatari inayoweza kuyakumba maisha yao, abiria na vyombo vyao.
Ni kwa msingi huo, abiria nao wanapaswa kujua kuwa, mlinzi wa kwanza wa usalama wao na familia zao ni wao wenyewe hivyo wasiruhusu madereva wasio makini kutumia ‘midomo na ndimi zao kuonja ubora wa sumu.’
Ndio maana tunasema wakati tunatoa pole kwa wote walioathirika na matokeo mabaya ya mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi za EAC, tunatoa mwito kwa wote wenye mapenzi mema zikiwamo taasisi na jumuiya za kimataifa kuwapa waathirika misaada ya hali na mali ili warudie hali zao za kawaida za maisha ya binadamu.
Kila mmoja kwa nafasi yake, achukue tahadhari kabla ya kufikwa na shari maana heri kinga kuliko kuponya.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa wale ambao tayari wamejenga maeneo hatarishi na wanafanya juhudi za kutoka, basi wasiwepo wengine wanaokwenda kujenga katika maeneo hayo yanayowafanya wao, jamii zao na serikali zao kuishi wakiwa na ‘roho mkononi’.
Pole kwa wana EAC wote waliokumbwa na athari za mafuriko, lakini wote tuchukue tahadhari maana kinga ni bora kuliko tiba.



