Tukemee wanaotaka kuleta vurugu uchaguzi mkuu

OKTOBA 29 mwaka huu Watanzania watakuwa katika hatua muhimu ya kupiga kura kwa ajili ya kuchagua rais, wabunge na madiwani ambao wataongoza nchi kwa kipindi cha miaka mitano. Ni kipindi muhimu kwa mustakabali wa maisha na maendeleo ya Watanzania kwani kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura anapaswa kushiriki kwenye hatua hiyo inayompa nafasi ya kuchagua kiongozi anayemtaka.

Wakati Watanzania wakisubiri kupiga kura Oktoba 29, mwaka huu, mchakato uliopo sasa ni kampeni za vyama vyote unaoendelea kwa wagombea kufanya mikutano ya hadhara kutangaza sera na ilani za vyama vyao lakini zaidi kutoa ahadi ambazo wanaeleza kuzitekeleza watakapoingia madarakani.

Kipindi hiki ni muhimu kwa Watanzania kusikiliza sera, ilani na ahadi za wagombea lakini pia kupima uwezo na weledi wa wagombea katika umahiri wa uongozi na namna ya kuvusha Watanzania kuelekea nchi ya ahadi.

Mchakato wa uchaguzi unaosimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) umekuwa ukiendeshwa kwa kuzingatia misingi ya Demokrasia kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi na wale waliokidhi vigezo vya kugombea walipata nafasi na kuendelea na mchakato.

Wakati huu ambapo siku chache zimebaki kuelekea kupiga kura, wapo watu ambao wamekuwa wakitoa maneno ambayo yanaashiria kuleta taharuki kwa Watanzania ikiashiria kutaka kuvuruga uchaguzi huo usifanyike. Kutofanyika kwa uchaguzi ni jambo kubwa sana ambalo halitaathiri serikali tu bali litaathiri maisha ya Mtanzania mmoja mmoja lakini pia litatuweka kwenye sura mbaya kwenye diplomasia ya kimataifa kama nchi wakati Tanzania inajulikana kama ‘Kisiwa cha Amani’.

Jambo hili halikubaliki na Watanzania tunapaswa kuungana na kupiga vita na kelele kwa nguvu kwa watu wote ambao wana nia ya kuleta vurugu kuelekea kuhitimisha uchaguzi mwaka huu. SOMA: Watanzania tusimamie misingi, utu wema kulinda amani ya nchi

Siku za hivi karibuni hapa mkoani Kigoma yalifanyika maulid ya kumswalia Mtume Muhamad (SAW) na mashehe na viongozi wakubwa wa dini kutoka mikoa mbalimbali ya nchi pamoja na mambo mengine walitoa kauli za kupinga kwa nguvu watu wote wanaotaka kuvuruga amani ya nchi kwenye uchaguzi mkuu.

Viongozi hao walienda mbali zaidi na kukemea kwa kueleza kuwa Watanzania wanapaswa kupiga vita jambo hilo na kutokubali kuungana na mtu yeyote mwenye nia ya kuvuruga uchaguzi huu kwani haina sababu za msingi kwa masilahi ya nchi.

Vyombo vya habari vina wajibu na ni mhimili mkubwa katika kutoa habari na kuelekeza maendeleo ya mchakato wa uchaguzi, hivyo ni vizuri waandishi na vyombo vya habari kujitenga na habari za uchochezi na zinazozua taharuki kwenye jamii.

Zaidi ya vyombo vya habari, kwa sasa kumekuwa na vyombo vya habari vya mtandaoni vinavyorusha na kuchapisha habari mbalimbali na vimekuwa na nguvu kubwa vikisambaa kwenye jamii. Tunayo mifano hai ya uchochezi uliosababisha kuvuruga amani ya nchi na Mkoa wa Kigoma ni moja ya mashuhuda wa hilo kwa kupokea idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi za ukanda wa maziwa makuu huku chanzo kikubwa cha vurugu katika nchi hizo ni siasa na ugomvi wa madaraka.

Tusikubali kuwa sehemu ya kuleta taharuki na mkanganyiko, tutumie vyombo vyetu vya habari na mitandao ya kijamii vizuri kwa kutoa elimu na miongozo ambayo itawapa nafasi Watanzaniaa kuamua kwa amani kuchagua viongozi wanaowataka.

Tanzania ni nchi huru na inafanya uchaguzi wake kwa kutumia sheria zake za nchi zilizotungwa bila kuingiliwa na nchi yoyote, hivyo tutii na kutekeleza sheria za nchi zinazosimamia uchaguzi ikiwemo kusimamia masuala ya ulinzi na usalama, kuepuka kufanya matukio ya uchochezi na jinai ambayo yanaenda kinyume na sheria za nchi.

Tunayo mifano hai ya uchochezi uliosababisha kuvuruga amani ya nchi na Mkoa wa Kigoma ni moja ya mashuhuda wa hilo kwa kupokea idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi za ukanda wa maziwa makuu huku chanzo kikubwa cha vurugu katika nchi hizo ni siasa na ugomvi wa madaraka.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button