Tumezima mwenge tumuenzi Nyerere

MWENGE wa Uhuru uliowashwa Aprili 2, 2025 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na kuzungushwa nchini ukiwa na Kaulimbiu, “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu” umezimwa Oktoba 14, 2025.

Hiyo ilikuwa Siku ya Kumbukizi ya Miaka 26 tangu Mwasisi wa Taifa, Mwalimu Nyerere alipofariki dunia, Oktoba 14, 1999 wakati akipatiwa matibabu jijini London, Uingereza. Kimsingi, kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kukumbusha na kuhamasisha Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaofanyika Oktoba 29, 2025 nchini kote.

Uchaguzi huu wa saba katika mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini, unafanyika takribani wiki mbili kabla ya siku ya upigaji kura baada ya Siku ya Nyerere ambayo pia ni kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Vijana. Aidha, sherehe za mwaka huu zimeenda sambamba na uzinduzi wa Kitabu cha Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Tanzania kilichoandikwa ili kuhifadhi kumbukumbu na chimbuko la mbio hizo nchini.

Wakiwa jijini Mbeya, viongozi mbalimbali wanasema kitabu hicho ni urithi na rejea muhimu, kwa kuwa kinakumbusha kuwa haki, usawa, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa uliopo, msingi wake ulijengwa na waasisi wa taifa kupitia Mwenge wa Uhuru.

SOMA: Dk Mpango: Tulinde amani kumuenzi Nyerere

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anawapongeza vijana waliokimbiza mwenge huo katika mikoa yote 31 nchini na halmashauri 195 kwa siku 195 mfululizo na kupitia miradi zaidi ya 1,382 ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ukisambaza ujumbe wa amani, umoja na uwajibikaji.

Anaitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha maudhui ya kitabu hicho yanafahamika na jamii nzima kupitia shule na vyuo. Mwaka huu, Dk Mpango amezindua Mbio za Mwenge wa Uhuru katika sherehe zilizofanyika mjini Kibaha Pwani na sasa Oktoba 14, mwaka huu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika sherehe za kuzima mwenge mkoani Mbeya.

Katika sherehe za kuzima mwenge huo zinazoenda sambamba na Kumbukizi ya Kifo cha Nyerere, Dk Mpango anasema Watanzania hawana budi kuungana kumuenzi Nyerere kwa kulinda na kudumisha amani. Anawataka kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kudumisha haki, usawa na kuzingatia matakwa ya wengi katika uamuzi Wilayani Kibaha,

Dk Mpango anasema uzalendo na juhudi za Nyerere ni mambo yaliyosaidia na kuwezesha Tanzania kupata Uhuru mwaka 1961. Anamtaja Nyerere kama mwanajumuiya wa kweli wa Afrika aliyeonesha uzalendo mkubwa kwa bara hilo.

default

Anapozungumzia Mwenge wa Uhuru, Dk Mpango anasema ulipoasisiwa ulilenga kuidhihirishia dunia na kuonesha maana ya taifa huru na uwezo wake wa kujitawala bila kuingiliwa. “Maono ya Mwalimu Nyerere yalikuwa sahihi, hasa kwa taifa ambalo ndio kwanza linajinasua kutoka katika makucha ya wakoloni,” anasema Dk Mpango katika sherehe hizo.

Ananukuu maneno, “Sisi tumekwisha uwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali penye chuki na heshima palipojaa dharau.”

Kwa mujibu wa Dk Mpango, falsafa hiyo ya Nyerere imekuwa dira ya mbio za mwenge kwa miaka yote, ikiendeleza dhamira ya kuhamasisha uzalendo na ujasiri wa kupambana na maovu katika jamii na kuleta amani, upendo, maendeleo na mshikamano katika taifa.

Katika maadhimisho hayo, Dk Mpango anasema falsafa hiyo imefanikisha mambo mengi nchini, likiwamo la kuondoa ubaguzi, ukabila na kujenga umoja wa kitaifa, kuimarisha utawala bora, kupinga dhuluma, dharau, chuki na kupambana dhidi ya ufisadi na rushwa.

Kuhusu maadhimisho ya wiki ya vijana, Dk Mpango anasema serikali imeendelea kuadhimisha Wiki ya Vijana Kitaifa, ili kutambua mchango wao katika ujenzi wa taifa. Anasema kupitia Maonesho ya Wiki ya Vijana yaliyofanyika Mbeya, vijana wameonesha uwezo mkubwa katika ujasiriamali na matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Sambamba na hayo, Dk Mpango alimwelezea Baba wa Taifa kama mtu wa mfano ambaye kila Mtanzania anapaswa kumuiga, hususani katika kujenga umoja wa kitaifa ili kuunda taifa imara. Kuhusu Kitabu cha Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Tanzania, anasema ni urithi na rejea muhimu kwa Watanzania.

Katika hotuba yake kwenye Sherehe za Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 mjini Kibaha Aprili 2, mwaka huu Dk Mpango anasema chimbuko la Mwenge wa Uhuru ni nia ya dhati ya Nyerere kuweka mwenge juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro kuleta matumaini, upendo na heshima kwa watu.

Anasema Nyerere alibainisha suala hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1959, akiwa New York, Marekani alipohutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Nyerere alimteua Alexander Nyirenda kutekeleza azma hiyo iliyoitwa ‘Operesheni Mwangaza’ ambapo yeye na wenzake walianza maandalizi Novemba 1961 kabla ya uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961.

Dk Mpango anasema, “Hatimaye usiku wa mkesha wa sherehe za Uhuru tarehe 9 Desemba 1961, Luteni Nyirenda na wenzake waliwasha na kusimika Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Tanganyika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, kama ishara ya kuwa huru…”

Anaongeza: “Kupandisha mwenge kileleni ilikuwa kwanza, ni kuonesha kazi ngumu iliyoko mbele ya kulijenga taifa changa la Tanganyika. “Pili, ilikuwa ni kuuwasha mwenge uangaze nje ya mipaka, kutoa matumaini pasipo na matumaini, upendo palipo na chuki na heshima palipo na uonevu na dharau…”

“Wazo la kukimbiza Mwenge wa Uhuru nchi nzima na kila mwaka lilitolewa na Vijana wa TANU (Chama cha Tanganyika African National Union) katika kikao kilichofanyika tarehe 26 Juni, 1964 lengo kuu likiwa ni kutekeleza kwa vitendo azma ya Baba wa Taifa ya kuhamasisha umoja, upendo, amani na ujenzi wa Taifa kwa kuhamasisha maendeleo.”

Anasema, “Tangu wakati huo, mwenge umekuwa ukikimbizwa katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupitia mbio hizo, hamasa kubwa imetolewa ili kuendelea kudumisha amani na kujenga uzalendo, umoja na mshikamano.” Anaongeza: “Katika kipindi chote hicho, mbio za mwenge zimekuwa na mafanikio makubwa yanayosadifu maono ya waasisi wa taifa letu.”

Katika maadhimisho hayo Mbeya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete anabainisha kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka ujao (2026), zitazinduliwa Zanzibar ambapo Mwenge wa Uhuru utawashwa na kukimbizwa nchi nzima.

“Tunapohitimisha mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, napenda kuutaarifu umma wa Watanzania kuwa uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 utafanyika katika Mkoa wa Kusini Pemba na maadhimisho ya kilele hicho katika kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ya miaka 27 na Wiki ya Vijana Kitaifa yatafanyika mkoani Rukwa,” alisema Ridhiwani.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni wilayani Mkalama, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya chama hicho, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi anasema Rais Samia ameonesha kwa vitendo kuenzi, kuthamini na kuendeleza urithi wa Baba wa Taifa, hivyo Watanzania wengine nao wafanye hivyo kustawisha taifa.

Dk Nchimbi ananukuu hotuba ya kwanza ya Nyerere ya Desemba 9, 1961 akikumbusha maneno ya Nyerere aliyetaja maadui wakuu watatu wa Tanzania yetu kuwa ni ujinga, maradhi na umasikini. Dk Nchimbi anasema, “Rais Samia amekuwa kiongozi anayeendeleza mapambano haya kwa vitendo kuimarisha huduma za elimu, afya na kukuza uchumi wa taifa letu.”

Dk Nchimbi alisema siku ya kumbukumbu ya Nyerere ni muhimu kwa Watanzania, kwani inawakumbusha misingi ya taifa, umoja na falsafa ya upendo aliyoiacha Nyerere.

“Tunaiheshimu kwa sababu ndiye muasisi wa uhuru wetu. Ndiye aliyeongoza vita ya uhuru wa Tanganyika kupitia TANU bila kumwaga damu na ndiye aliyeunganisha Tanganyika na Zanzibar kuwa taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” anasema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button