‘Tuongeze udhibiti wasio na vibali kufanya kazi nchini’

Wadau wa uvuvi Ziwa Tanganyika, wakiwa kwenye kikao

KIGOMA; Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amezitaka mamlaka za serikali zinazosimamia taratibu za kuingia nchini na kufanya kazi kwa raia wa kigeni kuondoa changamoto iliyopo ya idadi kubwa ya raia wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kuishi na kufanya kazi mkoani humo bila kuwa na vibali.

Andengenye amesema hayo akifungua mkutano wa wadau wa uvuvi wa Ziwa Tanganyika unaohusisha mikoa ya Katavi, Rukwa, Tabora na wenyeji Kigoma, ukiwa na lengo la kuzungumzia ulinzi, usalama na mkakati wa kuzuia uvuvi haramu katika ziwa hilo.

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya Kigoma, Salum Kali, amesema uwepo wa idadi kubwa ya raia wa kigeni wasio na vibali unatia shaka usalama wa nchi, lakini pia unaifanya serikali kushindwa kupanga mipango yake vizuri, kwani wapo watu wanaingia kwenye matumizi bila kuwepo kwenye mpango huo.

Advertisement

Salum Kali Mkuu wa Wilaya Kigoma, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Kigoma kwenye mkutano wa wadau wa uvuvi wa Ziwa Tanganyika(Picha zote na Fadhil Abdallah).

Kutokana na hilo alisema kuwa lazima wadau wote waungane kuhakikisha suala la raia wa kigeni kuishi na kufanya kazi nchini linadhibitwa, ikiwemo wamiliki wa vyombo vya uvuvi kuacha kuwatumia raia wa kigeni bila kufuata taratibu.

Akizungumzia kufanyika mkutano huo Kamisha wa operesheni na mafunzo wa jeshi la polisi, Awadhi Haji alisema kuwa kikao hicho ni mfululizo wa vikao ambavyo jeshi la polisi inavisimamia kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama wa Ziwa Tanganyika, lakini pia kuzungumzia masuala ya uvuvi haramu na uvunjaji wa sheria kwenye shughuli za uvuvi.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi nchini, Awadh Haji.

Awadhi alisema kuwa matumizi ya raia wa kigeni bila vibali na uvuvi haramu vinafanywa na watu mbalimbali, huku viongozi waliopo maeneo ya mwambao wa ziwa na bahari wanajua, lakini wanaficha, hivyo polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitaendelea kuchukua hatua kwa wote wanaoshiriki kwenye vitendo hivyo.

Katibu wa Chama cha Wavuvi Wilaya Kigoma, Mohamed Kasambwe alisema kuwa changamoto hiyo ipo kwa baadhi ya wamiliki wa vyombo vya uvuvi, ambao wanawatumia raia wa kigeni bila vibali.