‘Tupuuze taarifa zisizo rasmi Uchaguzi Mkuu’

DAR ES SALAAM: Shirika la Vijana na Wanawake (TAFEYOCO), limewaomba Watanzania kushirikiana na viongozi wao na kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa amani, likisisitiza umuhimu wa kuepuka taarifa zisizo rasmi kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 6, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa TAFEYOCO, Elvis Makumbo, amesema wananchi wana wajibu wa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi na kutumia kura zao kwa ufasaha.
“Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, tunao wajibu wa kushiriki. Tupuuze taarifa zisizo rasmi mitandaoni. Nafasi na utendaji wa viongozi unajulikana, tuungane na kuhakikisha tunajitokeza kupiga kura,” amesema Makumbo.
Pia amesema kuwa Watanzania wanapaswa kusikilizwa hasa pale wanapotoa hoja, ili kuepuka kuzuka kwa makundi yenye kupinga na kulalamika.
Kwa upande wake, Nasra Mussa, ambaye pia ni mwanachama wa shirika hilo, amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani akibainisha kuwa wanawake na watoto ndiyo waathirika wakuu panapotokea vita.
Naye Jolli Digalu, amehimiza wazazi kuwaonya watoto wao dhidi ya kutumia mitandao vibaya na kuchochea matusi ambayo hayana hoja.
“Watoto wetu wanapaswa kufahamu umuhimu wa amani. Tusiige mambo yasiyo ya maana,” alisema Digalu.