Tuzo ya TRA ni fursa kwa wabunifu inayolenga suluhisho la kodi
“MTU yeyote anayetoa taarifa sahihi kuhusu mkwepaji wa kodi atazawadiwa kati ya Sh milioni 1 hadi 20. Hii inakuwa fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika kulinda uchumi wa nchi.”
Anasema Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo katika ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Kodi linaloandaliwa na Chuo cha Kodi (ITA) hivi karibuni.
Katika kongamano hilo lililowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kodi na biashara, Nyongo anasisitiza jamii kutambua kuwa serikali inaendelea kuboresha miundombinu kwa kutumia mapato ya ndani.
Anasema ukwepaji wa kodi husababisha hasara kwa taifa, hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukwepaji huo kwa kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Naibu waziri anabainisha kuwa, TRA inatekeleza tuzo ya ubunifu inayolenga kuhamasisha wananchi, hususani vijana, kuwasilisha mawazo yatakayoboresha ukusanyaji wa kodi kwa njia rahisi, rafiki na bunifu ili kuongeza mapato ya serikali.
Kwa mujibu wa takwimu za TRA, tangu Julai 2024 hadi Februari 2025, mamlaka hiyo imekusanya Sh trilioni 21.2, ikilinganishwa na Sh trilioni 11.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2020/2021. Hili ni ongezeko la asilimia 78 na ukuaji wa asilimia 17. Aidha, marejesho ya kodi kutoka kwa wafanyabiashara ndani ya kipindi hicho yanafikia Sh trilioni 1.171 tofauti na Sh bilioni 92 miaka minne iliyopita.
Vyanzo mbalimbali vinasema TRA inatumia mifumo ya kisasa kama ‘TANCIS’ kwa shughuli za forodha na IDRAS kwa kodi za ndani kwa kuwezesha walipakodi kujihudumia wenyewe. Hali hii inapunguza uhusiano wa moja kwa moja kati ya walipakodi na maofisa wa TRA, hivyo kuongeza uwazi na ufanisi.
Ofisa Msimamizi Kodi Mkuu kutoka TRA, Kanuda Buluba anasema lengo la Tuzo ya Ubunifu wa Kodi si kushindanisha watu, bali hasa kupata mawazo bunifu ya kiendelevu na yanayotekelezeka. “Wazo lazima liwe jipya au liboreshe lililopo, liwe halijawahi kutekelezwa na mamlaka na liwe na faida kwa TRA,” anasema Buluba.
Vigezo hivyo ni pamoja na uhalisia wa wazo na manufaa yake kwa TRA, kuendana na mikakati ya mamlaka, urahisi wa utekelezaji kwa kutumia rasilimali zilizopo, kutotegemea teknolojia au mazingira ambayo hayapo nchini kwa sasa, pamoja na kuwa na rasilimali watu ya kutosha.
Kwa mujibu wa Buluba, zaidi ya mawazo 1,000 yanawasilishwa tangu kutangazwa kwa tuzo hiyo, na anawahimiza wabunifu wasikate tamaa kutokana na idadi hiyo kubwa.
Anasema zawadi zitakazotolewa kulingana na kiwango cha utekelezaji wa wazo husika ni asilimia 90 hadi 100 ya utekelezaji inayozawadiwa Sh milioni 50, asilimia 70 hadi 89 inazawadiwa Sh milioni 30 na asilimia 50 hadi 69 inazawadiwa Sh milioni 20. Maeneo yanayohitaji ubunifu ni huduma, mifumo, usimamizi na uendeshaji mzima wa TRA.
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi TRA, Paul Walalaze anasema mamlaka hiyo inaendelea kuboresha utoaji wa elimu kwa umma ili kuimarisha ukusanyaji wa kodi kwa hiari.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya kibiashara, kiuchumi na kijamii, mapato yatokanayo na kodi ndiyo huanzia, kuchochea na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii zikiwamo za elimu, afya, maji, barabara, umeme na miundombinu mbalimbali.
“Zamani watu walikuwa wakiwaona maofisa wa TRA kama watesi, lakini sasa wanapiga simu wakitoa taarifa za ukwepaji wa kodi kwa hiari. Hii ni hatua kubwa ya mafanikio kupitia elimu tunayotoa,” anasema Walalaze.
Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda anasema kongamano hilo limetoa jukwaa muhimu kwa mamlaka kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wadau, kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato ya serikali.
“Ni kupitia majukwaa haya, tunatambua maeneo yenye changamoto, yale tunayofanya vizuri na kubaini nini kifanyike ili kuongeza idadi ya walipakodi na kukuza biashara,” anasema Mwenda.



