Uanzishaji vituo kulea watoto vaiva Mbeya

MBEYA: MCHAKATO wa uanzishwaji wa vituo vya kijamii vya kulelea watoto katika maeneo yenye mikusanyiko jijini Mbeya umeanza rasmi baada ya uongozi wa halmashauri kwa kushirikiana na wadau kuainisha maeneo yatakayokuwa ya kwanza kuanzishwa vituo hivyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Anamery Joseph, maofisa ustawi wa jamii ngazi ya mkoa wa Mbeya na halmashauri pamoja na wadau kutoka mashirika ya Shalom Development Organisation(SHADO) na We Care Foundation.
Katika kikao hicho wadau kwa pamoja wameridhia maeneo ya masoko makubwa yawe ya kwanza kuanzishwa kwa vituo hivyo kwakuwa yana uhitaji mkubwa kwani watoto wengi wanakabiliwa na malezi duni pindi wazazi na walezi wao wanapokuwa kwenye shughuli za kuhudumia wateja wakati biashara zikiendelea.
Kaimu Mkurugenzi amesema jambo la uanzishwaji vituo vya kijamii vya kulelea watoto kwenye masoko linapaswa kupewa uzito ili kuleta ustawi wa malezi ya watoto kwa kuwapa haki zao za msingi katika ukuaji wao.
Joseph alimuagiza Ofisa Biashara wa Halimashauri ya Jiji hilo kutenga maeneo ya kufungua vituo vya malezi ya watoto katika masoko makubwa ikiwemo la Mwanjelwa, Sido, Soweto na Uyole.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Mtoto Kwanza kupitia Shirika la SHADO, Jenipher Antony amesema watoto waliopo katika masoko wanakosa malezi na uangalizi wa karibu kutokana na mazingira yaliyopo kutokuwa trafiki.



