“Uboreshaji miundombinu ya shule ni ajenda ya Rais”

KIGOMA: KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Ismail Ussi, amesema uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari ni ajenda kubwa ya Rais Samia Suluhu Hassan tangu siku ya kwanza madarakani.

Amesema lengo ni kurudisha hadhi na heshima ya shule za serikali ambazo zilikuwa zinakimbiwa na wananchi na kuwa na miundombinu duni.

Ismail Ussi amesema hayo leo Septemba 20, 2025 Mwenge wa Uhuru ulipozindua madarasa manne na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Ukombozi, Halmashauri ya Wilaya Kigoma ambapo amesema kutokana na hivyo serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imelifanyia jambo hilo kuwa la kipaumbele.

Ussi amesema Rais Samia alidhamiria kuondoa utofauti uliopo baina ya shule za serikali na shule binafsi za kulipia na kwamba hali hiyo imefanikiwa na sasa sehemu kubwa ya shule za msingi na sekondari za serikali zina miundo mbinu ya kujifunzia na kufundishia ambayo inawapa hamasa wananchi kupeleka watoto wao kwenye shule hizo.

Mmoja wa walimu wa shule hiyo, Anarei Mosha akizungumza na waandishi wa habari amekiri kuwa uboreshaji wa miundombinu katika shule hiyo umechochea wanafunzi kuhudhuria masomo sambamba na wazazi kusimamia watoto wao kuhakikisha wanafika shule.

Awali, Mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Thecla Pascal amesema kuwa kiasi cha Sh milioni 168.2 zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kupitia mradi wa kuboresha mazingira ya kujifundishia na kujifunzia chini ya Wizara ya Elimu (BOOST) na kutekelezwa kwa mradi huo kulilenga kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani katika shule hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button