Uchaguzi Mkuu 2025 watawala mahubiri mwaka mpya

DAR ES SALAAM; MAKANISA mbalimbali nchini yameendesha ibada ya kuukaribisha Mwaka Mpya 2025 huku viongozi wake wakitaka Watanzania kuombea taifa amani, uchaguzi mkuu, kujiimarisha kiimani na kuacha dharau na kiburi kwa kujishusha na kumnyenyekea Mungu.
Akizungumza kwenye mkesha wa mwaka mpya uliofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi alisema Watanzania wanapaswa kuliweka taifa mikononi mwa Mungu ili uchaguzi mkuu usifanyike kwa mazoea, hila na kwa namna yoyote isiyo na haki na ukweli.
Amewataka Watanzania kuombea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025, uwe wa haki, amani na utakaojali ustawi wa maendeleo ya taifa.
Pia, alisema ni mara ya 58 tangu Baba Mtakatifu kutangaza Januari Mosi ya kila mwaka kuombea amani duniani kwa kuwa wanafahamu kwamba kuna maeneo yameonja manyanyaso, dhuluma na umwagaji damu.
“Tunamuomba Mungu ayahurumie na kurehemu maeneo yote yenye vita, vurugu na umwagaji wa damu kwani maeneo hayo yanaashiria dhuluma, upendo na haki havishamiri na kwamba kama Watanzania tunajiita kisiwa cha amani, tunaomba tuwe wa kweli na wanyoofu,” alisema.
Kadhalika, alisema vipo vitendo ambavyo vimetekelezwa nchini Tanzania ambavyo haviashirii amani, havijengi mshikamano, upendo na havizingatii haki na ukweli.
Alisema wanapaswa kujenga amani katika mahusiano yao na wenzao, wakubwa na wadogo, wenye mamlaka na wasio na mamlaka kujenga amani ya kweli kwa wote na kwa kufanya hivyo watajenga ufalme wa Mungu.
Naye Kiongozi wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano, Kasisi Canon Jacob Kahemele ameonya wale wote wanaotafuta umaarufu na kudharau wengine, kushuka na kunyenyekea kwa sababu uhai walionao ni kwa neema tu.
Alisema hayo usiku wa kuamkia jana kwenye Misa ya Mkesha wa Mwaka Mpya wa 2025 katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano, Dar es Salaam.
Alisema kila mmoja ana mambo aliyopitia magumu na mepesi katika mwaka 2024 na kusema yote ni kumshukuru Mungu.
“Tutafanya bidii kuongeza upendo miongoni mwetu, tuishi maisha ya unyenyekevu, kusamehe, kutii neno la Mungu,” alisema.
Alisema anatamani wote waliopata baraka za Mungu kwa mwaka uliopita waendelee kunyenyekea na kushuka na kujali wengine.
“Tusisahau unyenyekevu, niwaonye wote wanaotafuta umaarufu shukeni, mnyenyekee, mmepewa neema tu msisahau hiyo ni baraka, mgeukieni Mungu aliyewapa hivyo na mjali na wengine,” alisema.
Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria wa Amani Jimbo Katoliki la Geita, Padri Revocatus Nchimila aliwataka waumini wa jimbo hilo kujifanyia tathmini kubaini ni mahali gani wamemkosea Mungu kwa mwaka uliopita kwa kutenda matendo mema, kuomba neema, waendelee kuishi maisha ya kiroho na baraka zaidi kwenye maisha yao ya kila siku.
Jijini Mwanza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akiwahutubia wakazi wa jiji hilo kwenye ibada ya mkesha wa Mwaka Mpya, aliwataka wakazi wa mkoa huo kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutekeleza majukumu yake kwa kumtanguliza Mungu.
Akizungumza kwa niaba ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza, Renatus Nkwande, Padri George Nzungu aliiomba serikali mkoani Mwanza kwa mipango yao kwa mwaka 2025 wajenge na kufanya upanuzi wa barabara ya kutoka mjini kati kuelekea Usagara wilayani Misungwi na ile inayotoka mjini kati kuelekea Nyanguge wilayani Magu ili kupunguza adha kwa watumiaji wa barabara hizo.
Akihubiri wakati wa ibada ya mkesha wa mwaka mpya, Paroko wa Parokia ya Kishogo, Jimbo la Bukoba, Padri Samuel Rwegoshora, aliwaasa waumini kuchagua viongozi sahihi katika uchaguzi mkuu ujao, ili wawaletee maendeleo endelevu huku akiwataka wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God (EAGT) Makoko, katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Paulo Kindamba aliwataka waumini na wananchi kutenga muda wa kuwa na familia zao, kwa kuwa na mshikamano katika familia ili kuepuka changamoto na vizuizi vinavyoweza kudhoofisha mafanikio yao katika maisha.
Msaidizi wa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa, Dean Chediel Lwiza akihubiri katika Kanisa la Azania Front, alitoa rai kwa wananchi kumshukuru Mungu kwa kuwapa baraka ya kuishi kwa sababu ndilo jambo muhimu kuliko kuwa na mali na utajiri wa aina yoyote.
“Mungu katika mwaka 2025 ametupa baraka ya kuishi, angeifuta angeiondoa usingekuwepo hapa, tunapoangalia baraka, angalia baraka ya kwanza ya familia, angalia baraka ya pili ya kuishi, amekulinda amekaa na wewe, wakati mwingine huwa tunasahau kama Mungu ametulinda sio kwamba tumejilinda, Mungu ametulinda,” alisema.
Lwiza alitoa wito kwa kila mtu kumthamini ndugu aliyenaye katika familia na ukoo wake kwa sababu kuwa na ndugu mwenye afya njema katika familia ni baraka pia, kwa kuwa kuna familia zimekosa baraka ya kuwa na ndugu zao wakiwa hai.
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Henry Mchamungu alikemea vijana kutoingia kwenye wito wa utawa kwa lengo la kukwepa majukumu, ugumu wa maisha na kukosa kazi.
Alisema utawa ni wito unaomtaka kijana kutofikiria kuingia kwenye ndoa, kuishi maisha ya ufukara na kutii viongozi wao.
Aliyasema hayo jana Dar es Salaam kwenye Misa Takatifu ya nadhiri za kwanza kwa masista wa Dada Wadogo wa Shirika la Mtakatifu Francisco, iliyofanyika katika Kituo cha Mbagala jimboni humo.
Misa hiyo ilihudhuriwa pia, na Askofu Mkuu, Juda Thadaeus Ruwa’ichi na Askofu Msaidizi, Stephano Musomba. Misa hiyo ilienda sambamba na maadhimisho ya Sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu inayoadhimishwa Januari Mosi, kila mwaka.
“Siku hizi watu wanamaliza shule hawana kazi, maisha ya mtaani ni magumu, anaweza akaamua kuingia kwenye utawa sababu ya kukwepa maisha,” alisema.

Alisema zipo sababu za watu kutaka kuwa watawa ili kujitenga na wengine na apate kuwa karibu na Mungu na kwa kufanya hivyo, watu wengine wanavutiwa na maisha hayo.
Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Ezekiel Mkamba amewataka waumini kujiimarisha kiimani kutimiza mipango yao mwaka 2025. Alisema hayo jana wakati wa ibada ya Mwaka Mpya iliyofanyika Kanisa la TAG Magomeni, Dar es Salaam.
“Mwaka 2025 ishikeni kweli ya Mungu, onesheni uhodari, msiwe legelege kuna mazingira yatakutaka usiwe legelege licha ya dhiki na taabu utakazokuta nazo, lakini kama ukiishika kweli ya Mungu utatimiza mipango na matarajio yako,” alisema.
Mkamba aliwataka wajifunze kasamehe hata kama umeudhiwa kiasi kikubwa, watubu pamoja na kujitafakari kila kukicha kama matendo yao yanampendeza Mungu.
Mchungaji wa KKKT Kijitonyama, Dk Eliona Kimaro ametoa rai kwa viongozi wa kisiasa, wananchi na wafanyakazi kuacha kiburi kwa sababu kiburi kinasababisha kukosa fursa nyingi.
Akizungumza wakati wa ibada ya mkesha wa mwaka mpya juzi Mchungaji Kimaro alisema kiburi cha madaraka kimezika ndoto za watu wengi.
“Kiburi cha madaraka kimezika mamia na maelfu ya watu wanaozikwa kwa vifo vya halaiki kwa sababu ya mtu mmoja amepewa nafasi ya kuongoza, lakini amekuwa na kiburi na kimezika watu maarufu,” alisema.
Imeandaliwa na Francisca Emmanuel (Dar), Ikunda Eric (Dar), Eva Sindika (Dar), Nashon Kennedy (Mwanza), Naziah Kombo (Mara), Abela Msikula (Bukoba), Rehema Lugono (Dar) na Yohana Shida (Geita).



