Ufukuaji mto waondoa athari za mafuriko Mbarali

MBEYA: JITIHADA zilizofanywa kufukua Mto Mambi ulioko Mbarali mkoani Mbeya zimerejesha furaha kwa wakazi wa vijiji vya Chamoto na Uhambule ambapo wameondokana na athari za nyumba zao kusombwa na maji na mazao kuathiriwa.

Wizara ya Maliasili na Utalii imetekeleza jitiada hizo kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

Ofisa Mtendaji Kijiji cha Chamoto Sekelaga Mwakapesa amesema urejeshaji wa kingo za maji na kufukua Mto huo umesaidia kuondoa adha hizo zilizowarudisha nyuma kimaendeleo.

Advertisement

Mwenyekiti wa Kijiji cha Uhambule Robert Kinanda ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi wa REGROW.

Mto Mambi ulipoteza uelekeo wake wa asili kutokana shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha Mwenyekiti wa watumiaji maji Bonde la Mto Mambi anayesimamia kata nne wilayani Mbarali, Japhet Mtafya amesema mradi wa REGROW umechimba kilomita 15 pamoja na kuongeza kina cha mto huo kwa gharama ya sh Milioni 200 kwa kutumia wataalamu wa ndani chini ya Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji na kuokoa zaidi ya sh Bilioni moja kama wangetumia wakandarasi wengine.

Katika kuhakikisha vyanzo vya maji wilaya ya Mbarali vinalindwa na kuwa na tija kwa wakazi wa kata ya Igurusi na maeneo jirani kupitia Mradi wa REGROW zimesimikwa alama za mipaka ‘beacon’ ili kuonesha mipaka ya kudumu ya vyanzo hivyo.