Uhamiaji Z’bar yapaisha mapato

SERIKALI imesema Idara ya Uhamiaji Zanzibar imeongeza wigo wa mapato yasiyo ya kikodi kutoka Sh bilioni 130 mwaka 2016-2020 hadi kufi kia Sh bilioni 323 mwaka 2021-2025. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene alieleza hayo wakati wa uwekaji jiwe la msingi la Chuo cha Mafunzo ya Uhamiaji Kitogani Kisiwani Unguja ikiwa ni shamrashamra kuelekea sherehe za Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Simbachawene amesema katika Miaka 62 ya Mapinduzi idara hiyo imepata mafanikio makubwa kiutendaji hasa katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki. “Uwepo wa mifumo ya kielektroniki ni chachu ya maendeleo yaliyofikiwa na idara ya uhamiaji Zanzibar na pia imeongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya serikali kufikia taasisi inayoongoza kwa kukusanya mapato yasiyotokana na kodi Zanzibar,” alisema Simbachawene.
Amesema mifumo hiyo imeongeza ufanisi katika usimamizi wa usalama wa mipaka ya nchi huku ikidhibiti kwa kiasi kikubwa watu wanaoingia na kutoka nchini. Alisema kwa sasa mifumo hiyo inatumika kutoa hati za kusafiria na vibali vya wanaotaka kuingia nchini, hali inayoongeza ufanisi katika ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi. SOMA: JK azindua jengo la Uhamiaji, makazi ya askari Pemba
Akizungumzia ujenzi wa chuo hicho, Simbachawene amesema kitakuwa nguzo ya maofisa wa uhamiaji kwani kitatoa mafunzo ya hali ya juu na kuboresha utendaji wao katika masuala ya uhamiaji hasa kuendana na mabadiliko ya teknolojia. Amesema chuo hicho kitazalisha askari wenye ujuzi, maarifa, weledi, uzalendo na nidhamu ili kuimarisha usalama wa mipaka na kusimamia maslahi ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema Idara ya Uhamiaji Zanzibar ina mabadiliko ya kiutendaji katika mikoa yote ya Zanzibar ambayo imeiweka Tanzania katika ramani nzuri kikanda na kimataifa katika masuala ya uhamiaji. Amesema chuo hicho kitatoa mafunzo ya kisasa yanayoendana na teknolojia na kutengeneza maofisa wengi wenye uwezo wa kudhibiti mipaka, usalama wa nchi, sheria za uhamiaji na kuheshimu haki za binadamu.



