Ujenzi Daraja la Magufuli wafikia 85%

MWANZA: Ujenzi wa Daraja la J.P Magufuli (Kigongo – Busisi) lenye Kilometa 3.2 pamoja na Barabara unganishi ya Kilometa 1.66, linalojengwa kuunganisha Barabara Kuu ya Usagara – Sengerema – Geita katika Ziwa Victoria umefika asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2024.

Taarifa hiyo imetolewa Machi 15, 2024 Mkoani Mwanza katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Kakoso ilipoambatana na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kukagua maendeleo ya mradi huo.

Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso ameeleza kuwa Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo na imempongeza Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha ili mradi huo ukamilike kwa muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za mradi huo kwa wakati ambapo mpaka sasa jumla ya Sh bilioni 441.3 zimetolewa kwa ajili ya kumlipa mkandarasi anayetekeleza mradi huo.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Doroth Mtenga ameeleza kuwa mradi huo unatumika kama darasa la mafunzo kwa wanafunzi na wataalamu wetu wa ndani kupata uzoefu wa kusimamia na kujenga madaraja mengine kama hayo hapa nchini.

 

Habari Zifananazo

Back to top button