Ulega aanika Samia anavyopiga kazi Ujenzi

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo – Saadani hadi Pangani, ni pamoja na Daraja la Mto Pangani, ni miongoni mwa kazi zinazoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Ulega ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja la Mto Pangani utahusisha kufunga taa 240 ili kuboresha miundombinu yake. Pia mji wa Pangani peke yake utawekwa jumla ya taa 200 na kufikia idadi ya taa 440 zitakazokuwa Pangani kuboresha miundombinu.
Ulega alisema daraja hilo ni mwendelezo wa kazi anayoifanya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga madaraja makubwa ambapo alipoingia madarakani amekamilisha madaraja nane nchini yanayowasaidia wananchi na kuwa hata mvua zikinyesha hawatakuwa na wasiwasi kwani wataendelea na shughuli zao.
“Madaraja hayo moja ambalo ni maarufu ni lile la Dar es Salaam la Tanzanite, lingine ni la Kitengule la Kagera lingine ni la Msingi pale Singida. Haya ni kati ya yale madaraja nane yenye thamani ya Sh bilioni 381, ambayo uliyakuta yakiendelea ukayakamilisha,” alisema Ulega.
Ulega alisema kwamba Rais Samia Suluhu Hassan alikuta barabara zinazoendelea kujengwa, kati ya hizo kilometa 1,366 zimekamilishwa kwa thamani ya Sh trilioni 2.7.
Alisema kwa ujumla, kilometa 2,031 za barabara zinaendelea kujengwa nchini zikiwamo zinazotoka Bagamoyo – Mkange – Tungamaa – Pangani na Tanga ni barabara ambayo ilipigiwa kelele na wabunge mbalimbali.
Alitumia pia fursa hiyo kumuahidi Rais kuwa wizara hiyo inasimamia kazi usiku na mchana bila kuchoka.
Amesema jambo la kufurahisha ni kwamba wakandarasi wa barabara hiyo hawaidai chochote serikali, badala yake wao ndio wanadaiwa.
“Wizara ya Ujenzi ikiwa inamdai mkandarasi, inamwambia asicheke wala ‘asi-relax’ afanye kazi usiku na mchana hadi kieleweke Watanzania wanaendelee kupata matunda ya uhuru wa nchi yao,” alisema Ulega.
“Daraja hili litaambatana pia umetuagiza tuweke taa za kutosha na ulisema katika kila barabara tunayoijenga katika taifa hili taa ziangaze, nuru iangaze na hapa Pangani nuru ya Rais Samia inakwenda kuangaza,” aliongeza Ulega.
Aliahidi kuwa Wizara ya Ujenzi itaendelea kusimamia kazi hizo usiku na mchana ili Watanzania wapate matunda ya maendeleo hayo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mohamed Besta alisema Barabara ya Bagamoyo, Makurunge Pangani – Saadani na Tanga iliyowekwa jiwe la msingi na Rais Samia jana, ina urefu wa kilometa 256 ikiwa ni pamoja na Daraja la Mto Pangani lenye urefu wa meta 525.

Alisema barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inaunganisha Tanzania na Kenya katika ukanda wa Pwani ya Mashariki ambapo utekelezaji wake unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na serikali.
Akifafanua juu ya utekelezaji wake, alisema umegawanyika katika sehemu mbili; ya kwanza ni ujenzi wa Barabara ya Tanga –Pangani kilometa 50 yenye gharama ya Sh bilioni 118.7, ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 75.
Sehemu ya pili ni ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa meta 525 ambalo linalogharimu Sh bilioni 107 na kwa sasa limefikia asilimia 53.
Sehemu ya tatu ni ujenzi wa barabara ya Tungamaa-Mkwaja-Mkange yenye kilometa 95 ikijuimisha pia barabara unganishi za Kikungwi inayogharimu kiasi cha Sh bilioni 123 ikijumisha gharama za usimamizi huku ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 46.
Sehemu ya nne ni ujenzi wa Barabara ya Mkurunge – Mukange kilometa 73 na mazungumzo yanaendelea.



