Ulega ataka mpango kazi kukabili foleni

DAR ES SALAAM; WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewaagiza mameneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha wanatengeneza mpango kazi utakaowezesha kukabiliana na changamoto ya foleni jambo linalochangia kuzorotesha shughuli za kiuchumi.
Hayo yamejiri wakati alipotembelea eneo la Kongowe lililopo mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya kutoka mbagala rangi tatu hadi Kongowe yenye urefu wa kilometa 3.8 iliyogharimu Sh bilioni 54.5.

‘’Serikali haiko tayari kuona wananchi wake wanashindwa kutekeleza kikamilifu shughuli za maendeleo kutokana na tatizo la foleni, ndugu zangu wakazi wa kongowe serikali yenu inatambua fika umuhimu wa eneo hili kuwa linakabiliwa na adha kubwa ya msongamano wa magari,’’amesema Ulega.
Ameongeza kuwa: ‘’Kutokana na uwepo wa changamoto hii imeamua kuwekeza mabilioni ya fedha kujenga barabara ambapo sasa magari yatakuwa yakipita bila bugudha, bila shaka kwahiyo kila mmoja wenu amejionea jinsi kazi zinavyoendelea”.
Aidha, Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutokana na heshima ya wanakongowe ameamua kuwaletea fedha za kujenga daraja la juu (Flyover) ili kuhakikisha magari yanapita kwa urahisi na wakati huo huo wananchi hao wakiendelea na shughuli zao za kiuchumi bila kikwazo chochote.

Ulega ametumia fursa hiyo kumwelekeza meneja wa TANROADS wa Mkoa huo wa Dar es salaam, Mhandisi Lazeck Kyamba kuhakikisha anaweka bango maalumu litakaloonesha taarifa za mradi huo wa ujenzi wa daraja ili wananchi waweze kuulewa.
Akijibu maombi ya wakazi wa eneo hilo yaliyowasilishwa na Adam Mkere kwa niaba ya wenzake kuhusu umuhimu wa kutengeneza barabara ya vicheji na ya kutoka mwembetegu hadi vikundu polisi ambapo amewahakikishia kuwa serikali inatambua changamoto hiyo na tayari imeweka bajeti kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo.
Pia amemwagiza mkandarasi wa mradi huo kutoka kampuni ya M/S Stecol Coparation ambaye mpaka sasa tayari ameshalipwa Sh. bilioni 8.1 fedha kwa ajili ya kufanya kazi hiyo usiku na mchana ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kuanza kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake meneja huyo wa TANROADS mkoani humo amemuhakikishia waziri huyo kuwa timu ya wataalamu iko makini kusimamia mradi kila hatua na maagizo yote yaliyotolewa ikiwemo kuhakikisha wazawa wanapewa kipaumbele cha ajira katika mradi yanatekelezwa.



