Umakini wahitajika habari za upotoshaji

DAR ES SALAAM: WAHARIRI na waandishi wa habari nchini wamehimizwa kuongeza umakini katika ukusanyaji na uchapishaji wa habari, hususan katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili kulinda demokrasia dhidi ya upotoshaji wa taarifa na habari bandia zinazotengenezwa kwa kutumia akili mnemba.
Akizungumza katika mafunzo ya siku mbili kwa wahariri na waandishi jijini Dar es Salaam, yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) Meneja Programu wa Baraza hilo Josephat Mwanzi, alisema baadhi ya taarifa za uongo zimekuwa zikisambazwa mitandaoni zikiwa na lengo la kuchafua taswira za watu na kuibua taharuki.
“Tuwe makini na maudhui yetu. Tunahitaji umakini mkubwa vyumbani mwetu vya habari, hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu,” alisema Mwanzi.

Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka Nukta Afrika, Daniel Mwingira, alieleza kuwa zipo njia mbalimbali za kubaini taarifa na picha zinazotengenezwa kwa akili mnemba, ikiwemo kuangalia chanzo cha taarifa, muda na mazingira ilipotolewa. Alisisitiza umuhimu wa kutumia majukwaa ya uhakiki kama vile Jamii Check kabla ya kusambaza taarifa zenye utata.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), William Shoo, alibainisha kuwa zaidi ya Watanzania milioni 37 wamejiandikisha kupiga kura, huku asilimia 85 ya wapiga kura hao wakitegemea vyombo vya habari, blogu na mitandao ya kijamii kupata taarifa sahihi.

Shoo alisisitiza kuwa maandalizi ya vyombo vya habari yanapaswa kuanza mapema angalau miezi mitatu kabla ya uchaguzi, kwa kuzingatia mafunzo ya uthibitishaji taarifa, uandishi wa habari za data, na uelewa wa sheria za uchaguzi.
Alikumbusha kuwa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 zinatoa masharti ambayo vyombo vya habari vinapaswa kuzingatia, akionya kuwa ukiukwaji wake unaweza kupelekea adhabu za faini au kifungo.

“Ni lazima tuweke mkakati wa kuthibitisha vyanzo, kushauriana na wataalamu na kufanya marekebisho ya haraka ya taarifa zisizo sahihi ndani ya saa mbili ili kuimarisha imani ya umma,” alisema.
Jaji Mstaafu Robert Makaramba alizungumzia kuhusu changamoto za “mamluki wa kidijiti” na akahimiza kujengewa utamaduni wa kitaifa wa kukabiliana na habari potofu.



