Umeme bwawa la Nyerere kufikishwa Dodoma

SERIKALI inaanza kutekeleza mradi wa kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma.
Taarifa ya Wizara ya Nishati imeeleza kuwa pia mradi huo utahusu upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vyenye uwezo wa kilovoti 400 vya Chalinze-Pwani na Zuzu-Dodoma.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi huo leo jijini Dodoma.
“Kutekelezwa kwa mradi huo kutawezesha umeme unaozalishwa katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) kusafirishwa hadi Dodoma kutokea kituo cha Chalinze mkoani Pwani, hali itakayosaidia kuboresha upatikanaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa,” ilieleza taarifa ya Wizara ya Nishati.
Iliongeza: “Mradi pia utaongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda mikoa yenye viwanda na migodi ya uchimbaji madini Kaskazini Magharibi, Kaskazini Mashariki, Kanda ya Kati na Kusini mwa Tanzania”.
Wizara hiyo ilieleza kuwa mradi huo unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 kwa gharama ya Sh bilioni 513. Ilieleza kuwa mkandarasi wa mradi huo ni M/s TBEA CO. LTD kutoka China.



