UN yataka uchunguzi machafuko Angola

LUANDA, ANGOLA : UMOJA wa Mataifa umetaka kufanyika uchunguzi wa haraka, wa kina na huru kufuatia machafuko ya siku mbili nchini Angola yaliyoambatana na uporaji na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20.
Machafuko hayo yalizuka Jumatatu wiki hii baada ya maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta lililotangazwa Julai 1, hatua iliyozua hasira kwa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta lakini linalokabiliwa na kiwango kikubwa cha umaskini.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Thameen Al-Kheetan, amezitaka mamlaka nchini Angola kuchukua hatua za haraka kuchunguza vifo hivyo pamoja na tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa maandamano hayo.
Mpaka sasa zaidi ya watu 1,000 wamekamatwa na kuwekwa kizuizini kufuatia ghasia hizo ambazo zimeelezwa kuwa mbaya zaidi hazikuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.
Mamlaka nchini Angola bado hazijatoa taarifa ya kina kuhusu vifo hivyo, huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakitoa wito wa kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji kwa vyombo vya dola. SOMA: Bei ya mafuta yazua ghasia Angola
Angola, licha ya kuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta barani Afrika, imekuwa ikikumbwa na changamoto za kiuchumi, ukosefu wa ajira na mfumuko wa bei, hali inayochochea hali ya sintofahamu miongoni mwa wananchi.



