WATOTO zaidi ya 1,700 waliokuwa wamefikishwa vituo vya polisi kwa makosa madogo badala ya kufikishwa mahabusu gerezani walichepushwa na kupelekwa katika uangalizi wa jamii na wamekuwa ni watoto wenye tabia njema.
Ofisa Ulinzi wa Watoto wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF),nchini Joseph Matimbwi amesema hayo mjini Morogoro akitoa salamu za mwakilishi wa shirika hilo nchini katika ufunguzi wa mafunzo ya Ulinzi na usalama wa mtoto kwa maofisa na askari wa mapokezi wa Jeshi la Magereza ambao wanasimamia watoto magerezani .
Matimbwi ambaye pia ni Mratibu wa Program ya Community rehabilitation Project amesema kuwa program hiyo ilianza mwaka 2013 katika mikoa miwili ya Dar es Salaam na Mbeya na mwaka 2016 ikaenda katika baadhi ya mikoa mingine nchini.
Amesema Programu hiyo inahusika na watoto wale ambao hawafikishwi gerezani na imewasaidia watoto wengi ambao wametoka kwenye uhalifu na wamerudi kwenye jamii wakiwa ni wenye tabia njema.
“ Tangu Program hii ilipoanza katika baadhi ya mikoa nchini imewezesha mamia ya kuchepushwa na kurudishwa tena kwenye tabia nzuri ,wengine wamerudishwa shuleni na kwa wazazi wao ambao wanaendelea na tabia njema,” amesema Matimbwi.
Amesema programu hiyo imewasaidia watoto wengi wametoka kwenye uhalifu na wamerudi katika jamii na baadhi wamekuwa ni mafundi wazuri kwenye fani mbalimbali ambao wanatumiwa na jamii.
Matimbwi amesema Unicef ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Jeshi la Magereza katika kuona utofauti wa mtoto utakaoweza kuneemesha ustawi wake zaidi ambao anauhitaji.
“ Nalishukuru Jeshi la Magereza kwa kutoa mafunzo haya kwa Maofisa na askari ambayo yataleta faida nyingi ambazo watoto watazipata kwa Tanzania nzima kwa maendeleo yao ambao pia ni taifa la kesho ”amesema Matimbwi.
Naye Kamishna wa Magereza ,Nicodemus Tenga ( Divisheni ya Sheria na Uendeshaji) kabla ya mgeni rasmi amesema Jeshi la Magereza linapokea mfungwa au mahabusu kwa amri halali ya vyombo ambavyo kihalali vimeruhusiwa na sheria, kanuni na taratibu za nchi kuwaleta watu gerezani.
Tenga alisema Jeshi hilo halina mamlaka ya kumleta mtu gerezani ,bali mamlaka yake ni kumpokea kumhifadhi ,kumlinda ,kumpa huduma na kumrekebisha.
Kwa upande wa Mgeni rasmi ,Kamishna wa Magereza ,Bertha Minde (Huduma za Urekebu) amesema mafunzo hayo ni ya muhimu kwao katika kuhakikisha watoto waliopo magerezani wanapata ulinzi na usalama unaohitajika.
Minde amewataka maofisa na askari wa ulinzi na usalama wa mtoto kuhakikisha watoto waliopo magerezani wanapata huduma bora na mazingira salama,na mafunzo hayo yatawasaidia kuwa na mbinu bora za usimamizi wa watoto.