Unywaji maziwa bado uko chini ya 50%

GEITA: BODI ya Maziwa Tanzania (TDB) imesema wastani wa kiwango cha unywaji wa maziwa kwa kila mtanzania bado ni lita 68 sawa na asilimia 34 ya kiwango elekezi cha lita 200 zinazoshauriwa kitaalamu.

Hatua hiyo imeifanya TDB kuanzisha kampeni maalumu ya kuhamasisha unywaji wa maziwa katika shule na vituo vya kulelea Watoto ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya maziwa kwa mwaka 2025.

Ofisa Mteknolojia wa Chakula Mwandamizi wa Chakula kutoka TDB, Deogratius Buzuka amesema hayo walipofika kugawa maziwa katika vituo vya kulelea Watoto wa AIC Yeriko na Moyo wa Huruma mjini Geita.

Buzuka amesema bado kuna mwitikio mdogo wa unywaji wa maziwa wa makundi yote kuanzia Watoto hadi wazee tofauti na maelekezo ya Shirika la Afya Dunia (WHO) na Shirika la Chakula Duniani (FAO).

Amesema hiyo imetokana na watanzania wengi kula kwa mazoea hali inayopelekea udumavu wa mwili na akili ya Watoto wengi na hivo kuwa na miili dhaifu na uelewa mdogo shuleni na katika mazingira.

Amesema kwa kulitambua hilo TDB katika kuadhimisha wiki ya unywaji wa wanahamasisha wanafunzi kuhusishwa kunywa maziwa chini ya kauli mbiu ‘Kwa Matokeo Mazuri, Maziwa Ndiyo Mpango Mzima.

“Kwa hiyo tuhakikishe tunatumia maziwa ya kutosha, tusikariri kwamba maziwa ni kwa ajili ya Watoto wadogo tu wanaokua, maziwa ni kwa ajili ya rika zote”, amesema Buzuka.

Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Geita, Casian Luoga amesema kama mkoa wamejidhatiti kuhamasisha shule na vituo vya kulelea Watoto wanalipa kipaumbele suala la unywaji wa maziwa kwa afya ya mwili na akili.

“Serikali imeamua kuleta maziwa kwa wanafunzi ili wawe na afya bora, waweze kuwa na afya bora, kufaulu vizuri na kukua vizuri kwa sababu nyie ni viongozi wa kesho, tunataka taifa lenye uwezo mkubwa” amesema.

Mratibu wa Kituo cha AICT-YERIKO, Methusela Jackson amesema kituo kinalea na kufundisha watoto 203 kati yao wavulana 101 na wasichana 102 ambao wengi wao ni chini ya umri wa miaka 10.

Amesema tathimini inaonyesha bado wana uhitaji mkubwa wa maziwa kwa watoto kwani wengi wao bado wapo hatua ya ukuaji inayohitaji lishe bora ikiwemo maziwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Moyo wa Huruma, Sister Maria Lauda amesema kituo hicho kinalea watoto 165 ambo wapo kwenye hatua tofauti za umri na elimu na wamepanga kufuga ng’ombe wa maziwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button