“Uongozi uitishe kikao cha dharura na kupanga utaratibu wa kulipa deni”

ARUSHA: LICHA ya Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 100, bado kuna changamoto kubwa ya matumizi ya fedha hizo, huku watumishi wakidai jumla ya Sh milioni 980.
Hayo yamesemwa na Mkaguzi wa Nje Mkoa wa Arusha, Valence Rutakyamirwa wakati wa ukaguzi wa hoja 12 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kwa mwaka 2023/24 ambapo halmashauri hiyo imepata hati safi.

Amesema hali hiyo si tu inazorotesha morali ya watumishi bali pia inakiuka haki zao za msingi na kusisitiza kuwa kuna haja ya halmashauri kupitia upya vipaumbele vyake vya matumizi na kuhakikisha madai ya watumishi wanalipwa kwa haraka kupitia fedha kutoka hazina.
“Ni jambo lisiloeleweka kuona halmashauri imefikia lengo la mapato kwa asilimia 100, lakini bado kuna madai ya Sh milioni 980 kwa watumishi, tunashauri uongozi uitishe kikao cha dharura na kupanga utaratibu wa kulipa deni hili kupitia fedha zinazopatikana,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Missaile Musa, alihoji kwani ni zaidi ya Sh bilioni 4.5 za miradi ya maendeleo hazijatumiwa na halmashauri hiyo, fedha ambazo zilipaswa kuelekezwa kwenye sekta muhimu kama afya, elimu na miundombinu ya kijamii.
“Fedha hizi zilitolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati, lakini hadi sasa hazijaingizwa kwenye matumizi. Hili ni jambo linalozua maswali makubwa na linaweza kuchelewesha ustawi wa wananchi wa Monduli,” ameongeza.
Amesema ucheleweshaji huo unaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwataka viongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kwa haraka na kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi katika sekta za elimu na afya.



