Upatikanaji dawa vituo vya afya wafikia 87%

SERIKALI imesema hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vyote vya afya nchini umefikia asilimia 87 na kwenye Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) ni zaidi ya asilimia 77. Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema haya kwenye televisheni ya Azam wakati akieleza hali ya upatikanaji wa dawa na fursa za uwekezaji wa viwanda vya bidhaa za afya nchini.

Ameeleza kuwa hali hiyo inachangiwa na ongezeko la bajeti ya dawa katika kipindi cha miaka mitatu ambayo imeongezeka kutoka Sh bilioni 200 hadi Sh bilioni 398, hadi sasa zaidi ya Sh bilioni 198 zimeshapelekwa MSD kwa ajili ya ununuzi wa dawa. “Hali ya upatikanaji wa dawa nchini ni nzuri lakini kwa sasa Tanzania inaagiza kiasi kikubwa cha dawa kutoka nje ya nchi, sawa na asilimia 80 kwa dawa za kawaida, dawa maalumu mfano za maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) ni asilimia 100, vifaatiba asilimia 90 na vitendanishi vya maabara asilimia 99,’’ alisema Msasi.

Amesema katika kutimiza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kwamba ifikapo mwaka 2030 Wizara ya Afya ihakikishe uagizaji dawa nchini uwe umefika chini ya asilimia 50, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa anatarajia kukutana na wawekezaji wa viwanda vya uzalishaji wa vifaatiba wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujadiliana mabadiliko makubwa ya kisera ya uwekezaji nchini.

Msasi amesema serikali inafanya hivyo vyote kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inakuwa ni kitovu cha dawa na vifaatiba katika nchi za Kanda ya Afrika na Jangwa la Sahara. Amesema kupitia uhamasishaji wanaoufanya kwa wawekezaji, wanatarajia kupata wawekezaji wa kuzalisha malighafi zinazotumika kutengeneza bidhaa za afya.

Amebainisha kuwa ili kuwa na kiwanda kikubwa cha kuzalisha kiini cha dawa, lazima hali ya viwanda vya uzalishaji nchini iwe juu, hivyo kupitia uhamasishaji wanatarajia nchi kuwa na viwanda vingi ambavyo vitachangia kuvutia wawekezaji wa viwanda vinavyozalisha viini vya dawa nchini. “Dawa muhimu ambazo zinatibu magonjwa ya wagonjwa wote nchini, hizo tumefanya tathmni ya kwanza ambayo ilifanyika mwaka 2022, tukabaini tulikuwa na uwezo wa kuzalisha baadhi ya vifaatiba kupitia viwanda vilivyopo,’’ alisema.

Amesema kwa sasa Tanzania inazalisha baadhi ya dawa ikiwemo za maumivu, malaria na za kuua bakteria, sindano, mabomba ya sindano pamoja na bidhaa nyingine zinazotumika hospitali. SOMA: MSD yafikia 80% usambazaji vifaa tiba, dawa

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button