Utaratibu usajili Mwambao Marathon watajwa

WAANDAAJI wa mbio za TASWA Mwambao Marathon, wametoa utaratibu wa kujisajili kwa wanaotaka kushiriki mbio hizo zitakazofanyika Desemba 22, 2024 mkoani Tanga.

Taarifa ya Kaimu Katibu Mkuu wa TASWA, Imani Makongoro imesema, kampuni ya simu za mkononi ya Tigo imewapa namba maalum kwa ajili ya wanamichezo kujisajili katika mbio hizo.

Malengo ya mbio hizo, mbali na kuboresha afya, ni pamoja na kuunga mkono mkakati wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi kupitia michezo na wanamichezo.

Makongoro amesema namba hiyo itawawezesha washiriki kujisajili, kuchagua mbio wanazotaka kukimbia na kulipia ada ya ushiriki.

Isome pia: TASWA Mwambao Marathon sasa Des.22

Amesema kuwa kutakuwa na mbio za kilomita 5, 10 na 21, ambapo kila mshiriki atalipia kiasi cha shilingi 30,000 tu kwa mbio anayotaka kushiriki.

“ Tunawashukuru sana wadau wetu Tigo kwa kufanikisha zoezi hili muhimu ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kuhamasisha nishati safi hapa nchini kupitia michezo,” amesema Makongoro.

Amesema wakati wa mbio hizo, TASWA itawahamasisha wanamichezo kutumia nishati safi ya kupikia kwa kuwa michezo ina ushawishi mkubwa katika jamii ili kusaidia mpango wa Serikali wa kuhakikisha hadi kufikia 2034 angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

“Hatua za kujisajili mshiriki ataingia kwenye menu ya Tigopesa ambayo ni *150*01# halafu atabofya namba 5, baadaye namba 6, kisha namba 1, itafuata namba 5 na baadaye namba 3 na atachagua tiketi ya kushiriki mbio anayoitaka na kulipia kupitia LIPA NAMBA 0777333110 ya Taswa Mwambao Marathon,” amesema.

Makongoro ametoa wito kwa kampuni, mashirika, taasisi na watu binafsi kujitokeza na kusaidia mbio hizi ili kuisapoti Serikali katika kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ili kumtua ‘mama’ kuni kichwani na kutunza mazingira.

 

Habari Zifananazo

Back to top button