“Utekelezaji miradi utaipa ushindi CCM”

KIGOMA: Mgombea ubunge Jimbo la Kasulu Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Joyce Ndalichako amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi uliofanywa na serikali ya awamu ya sita unawafanya wagombea wa chama hicho kuamini watashinda Uchaguzi Mkuu.
Prof Ndalichako amesema hayo katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi uliofanyika kijiji cha Ruhita Wilaya ya Kasulu ambapo alisema kwa miaka mitano aliyokuwa mbunge jimboni hapo kazi kubwa imefanyika ambayo imeiweka serikali kwenye mioyo ya watanzania.
Alisema kabla ya mwaka 2020 jimbo hilo lilikuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara lakini kazi iliyofanyika kwa sasa imefanya barabara za jimbo hilo kupitika zikiwemo barabara za lami huku shule mpya tisa za sekondari na sita za msingi zikijengwa.

Akieleza kuhusu miradi ya maji alisema kuwa ipo miradi mbalimbali midogo ilitekelezwa na kupunguza changamoto ya maji kwa wananchi wa jimbo hilo ambapo kwa sasa serikali inamalizia mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Sh bilioni 35 ambao utaondoa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Akizungumza katika uzinduzi huo wa kampeni Katibu wa CCM Mkoa Kigoma, Christopher Pallangyo amewataka wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani mkoani humo kutumia ilani ya uchaguzi ya CCM kwani imesheheni mambo makubwa ambayo chama hicho kimeelekeza kufanywa na serikali mambo ambayo yanagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Pallangyo alisema kuwa haina maana kutumia nguvu kujibu mambo ya hovyo yanayozungumzwa na wapinzani kwani mambo yaliyofanyika vipindi vilivyopita katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM yanapaswa kuwa ajenda kubwa ya wagombea wakieleza yaliyofanywa na serikali hivyo wagombea wanapaswa kujivunia ilani hiyo.



