UTI yatumiwa vibaya kujipatia mapato

JAMII imetakiwa kupewa elimu ya kutosha kuhusu maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) ili kuepuka matumizi holela ya dawa yanayosababishwa na baadhi ya hospitali kutaka fedha.
Wito huo umetolewa na Dk Halifa Nkumbi wa Zahanati ya Muzidalfa Islamic Charitable Organization iliyopo Sinza, Dar es Salaam, wakati akizungumza na gazeti la HabariLEO.
Alisema maambukizi ya UTI yamekuwa chanzo cha mapato kwa baadhi ya hospitali hasa za binafsi, ambapo hupata kipato kutokana na vipimo visivyo sahihi kuonesha UTI.
Alisema hospitali za serikali hazina tatizo hilo kwa sababu vifaa vinatayarishwa kwa usafi unaotakiwa.
Alisema vimelea vinavyosababisha UTI haviwezi kukaa mwilini zaidi ya wiki mbili au tatu bila kuleta madhara, hivyo si kweli kwamba kila mkojo mchafu ni UTI.
Taarifa kuhusu UTI zilisambaa zikidai asilimia 80 ya waathirika ni wanawake, kutokana na bakteria kuhamia kutoka sehemu ya haja kubwa na kuingia katika njia ya mkojo kuanzia kwenye mrija wa urethra, kibofu cha mkojo hadi kwenye figo.
Sababu nyingine ni usafi duni, tabia za ngono zisizo salama kwa wanawake, matumizi ya nguo za ndani zinazotengeneza joto na unyevu kama nailoni, kukaa na mkojo kwa muda mrefu, na kushindwa kunywa maji ya kutosha.
Alieleza UTI ni maambukizi yanayosababisha maumivu wakati wa kukojoa, homa za muda mrefu na kuumwa mwili. Hata hivyo, watu wengi hupata matokeo ya vipimo vya UTI bila kuzingatia muda na usahihi wa uchukuaji sampuli.
Katika kipindi hicho, alisema mkojo huwa na uchafu wa asili kama damu ya hedhi, hivyo majibu huonesha mkojo mchafu na wagonjwa hutibiwa majibu badala ya ugonjwa halisi.
Aliongeza kama mtu angekuwa na UTI sugu inayoharibu figo, basi figo zingeharibika, jambo ambalo si mara kwa mara linaonekana.
Daktari huyo alisema jamii imeaminishwa vibaya, jambo ambalo limefanya baadhi ya wagonjwa kudai dawa za UTI wanapopewa viuavijisumu vya magonjwa mengine bila kuelewa dawa hizo zinaweza kutibu magonjwa zaidi ya moja.
Aidha, aliitaka jamii kuelimishwa zaidi kupitia wataalamu wa afya na vyombo vya habari, ikiwemo vipindi
vya redio na televisheni ili kuondoa imani potofu.



