USHIRIKISHWAJI na uwajibikaji katika jamii ni njia pekee itakayosaidia kupambana na magonjwa ya milipuko na majanga kabla na baada ya kutokea.
Jamii inahimizwa kufuata taarifa zinazotolewa na mamlaka husika za Wizara ya Afya na TAMISEMI kusaidia kujikinga na kukabiliana na magonjwa ya milipuko ya kupindupindu, M-Pox na kuyatokomeza.
Ofisa anayehusika na ushirikishwaji na uwajibikaji kwa jamii kutoka Tanzania Red Cross society (TRCS) Sara Warioba anabainisha jinsi Tanzania Red Cross society inavyojiandaa kukabiliana na magonjwa ya milipuko na majanga kabla na baada ya kutokea.
“Tunafuata miongozo ya serikali hatuwezi kufundisha pasipo kufuata miongozo hiyo kupitia Wizara ya Afya na TAMISEMI maana hao voluntia wetu wako ndani ya ngazi ya jamii,”amesema Warioba.
Anafafanua kuwa taarifa zinazofanyiwa kazi na Red Cross kupitia voluntia ni taarifa zilizotolewa na kuthibitishwa katika ngazi ya mkoa na ngazi ya Wizara ya Afya na sio kukurupuka.
Sara amesema kuwa mafunzo yanasaidia kuelimisha jamii na wanahusisha jamii kubaini chanzo cha ugonjwa na mbinu za kukabiliana nazo kwa pamoja.