Veta yaja kibiashara, kutumia vituo 14 vya umahiri

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeanzisha kampuni ya kibiashara.

Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa kuhusu mafanikio na mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Kasore amewaeleza waandishi wa habari Dodoma kuwa kampuni hiyo itakuwa ikifanya kazi za kubiasharisha ubunifu, bidhaa na huduma za Veta.

Alisema kampuni hiyo imeshasajiliwa kwa Hati Na. 177837210 na imekamilisha taratibu za kuanza kutoa huduma kupitia kandarasi mbalimbali.

“Lengo la kuanzisha kampuni tanzu ni kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini,” alisema.

Aliongeza: “Vilevile kampuni itatoa fursa zaidi za wanafunzi kushiriki mafunzo ya vitendo na hivyo kupata uzoefu na kukuza mitizamo na mbinu za ujasiriamali kwa wanafunzi na wahitimu wa vyuo vya Veta.”

Kasore alisema Veta imeandaa mkakati na kuanza kutekeleza kutoa mafunzo yanayoelekea kwenye tunuku za kimataifa.

“Hii ni kutokana na takwimu kutoka kwenye Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwa kuna jumla ya miradi 1,188 iliyosajiliwa na kutoa ajira 345,464 kwa kipindi cha mwezi Machi 2021 hadi Machi 2024,” alisema.

Aliongeza: “Tutafanya hivyo kupitia vituo vya umahiri na tumepanga kuwa na vituo kumi na vinne vya umahiri nchini kote. Kwa sasa tumefanya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya fani ya uchomeleaji na uungaji vyuma vyenye gharama ya Sh bilioni 1.773”.

Kasore alisema Veta itaimarisha ushirikiano na vyuo vya nchi nyingine na wabia wa maendeleo. Alisema ushirikiano huo unalenga kubadilishana uzoefu na kujenga uwezo kwa wakufunzi, kupata vifaa vya kisasa vya mafunzo na
kukuza mbinu za kisasa za ufundishaji na ujifunzaji.

“Miongoni mwa nchi tutakazoendelea kushirikiana nazo ni pamoja na China, Uingereza, Korea ya Kusini, India, Scotland na Ujerumani.

Wabia wa Maendeleo tutakaoendelea kushirikiana nao ni pamoja na GIZ, Koica, Benki ya Dunia, Unesco,” alisema
Kasore.

Alisema wameanzisha mpango wa Veta na Fundi Mahiri wakishirikiana nao kutoa mafunzo na shughuli za uzalishaji.

Kasore alisema wanafunzi wao pia wanapangiwa muda wa kwenda kupata mafunzo kwa hao mafundi mahiri wakati wa mafunzo kwa vitendo.

“Mafundi mahiri pia wanapata fursa ya kupata ujuzi zaidi kupitia karakana zetu na wengine kurasimishwa ujuzi wao kwa kupatiwa vyeti. Vilevile mafundi mahiri wanapewa nafasi ya kutoa mafunzo vyuoni na kushiriki katika kutathmini mafunzo ya vitendo wakati wa utahini,”alisema.

Kasore alisema Veta inashirikiana na kampuni na waajiri zaidi ya 100 kwa ajili ya kutoa mafunzo ya vitendo mahali pa kazi.

Alisema mamlaka imefanya tathmini ya mahitaji ya ujuzi katika shughuli za kiuchumi na kijamii zinazofanyika kwenye mikoa na wilaya zote nchini.

Alisema itaendelea kufanya hivyo kuhakikisha ujuzi unaohitajika unatolewa kwenye vyuo vya vya ufundi stadi kwenye mikoa na wilaya zote.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button