Vijana 23,460 warasimishwa nje ya mfumo rasmi wa elimu

DAR ES SALAAM: MAMKALA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imerasimisha ujuzi wa vijana wa Kitanzania 23,460 walio nje ya mfumo rasmi wa elimu, hivyo kuwapa sifa na vigezo vya kuajirika na kutambulika rasmi.

Aidha VETA kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wamerasimisha ujuzi wa wafungwa 214 katika mageraza yaliyo kwenye kanda tatu nchini.

Hatua hiyo ni moja ya mkakati wa serikali wa kuhimiza uwekezaji kwenye ujuzi bila kikomo ili kupata stadi za maisha na kuzitumia kujiajiri au kuajirika.

Afisa Utahini na Utunuku wa VETA,Rhoda Mgaya alisema hayo Dar es Salaam kwenye kongamano la elimu linalohitimishwa jana, ikiwa ni sehemu ya madhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima(TEWW)yaliyofanywa sambamba na maonesho ya ujuzi na stadi za maisha.

“Serikali inatambua umuhimu wa Watanzania kuwa na ujuzi kama sehemu ya kuongeza stadi za maisha ili kuhakikisha watu wanajipatia kipato cha ziada kupitia ujuzi na hivyo kukuza Uchumi,”alisema Rhoda.

Alisema kupitia VETA wameunga mkono juhudi ya kutoa mafunzo nje ya mfumo rasmi kupitia Programu ya Kurasimisha Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo Rasmi (RPL).

Alisema VETA inatambua kuna mafundi wengi mahiri wenye ujuzi kutoka sehemu mbalimbali za kazi ambao wameupata kwa uzoefu wa kufanya kazi au kurithishwa na wana mchango mkubwa hivyo kupitia programu hiyo wamerasimishwa ujuzi wao na kutambukika rasmi.

“ Kupitia program hiyo vijana 23,640 wa fani 10 tofauti wamerasimishwa kuanzia mwaka 2006 hadi 2025 hivyo kutambuliwa rasmi,”alisema Rhoda.

Alitaja fani hizo kuni ni fundi magari, useremala, uungaji na uundaji vyuma ,umeme ,ushonaji, uandaaji na upishi wa vyakula, mauzo ya vyakula na vinwaji, uundaji na utandazai bomba, bodi za magari na uashi .

“Vijana wanatamani kupata ajira ,wana ujuzi ila kikwazo ni hawana vyeti tunawaibua kupitia program hiyo ya RPL na kuwapima umahiri walionao na kuwaongezea ujuzi maeneo yenye upungufu na kisha kuwatambua na kuwapa vyeti,”alisema Rhoda.

Aidha alisema VETA kwa kushirikiana na TEWW wanatoa mafunzo nje ya mfumo rasmi ili kuwasaidia vijana watambulike na kuajirika.

Alisema katika eneo hilo, wameendelea kupanuka zaidi kwa kuongeza ushirikiano taasisi nyingine wakiwemo Jeshi la Magereza ambalo mwaka jana wamerasimisha ujuzi wa wafungwa 214 katika magereza ya kanda tatu.

Kanda hizo ni Mashariki, Kaskazini na Kanda ya Dar es Salaam na ujuzi huo umeangukia kwenye fani tofauti 10 zilizotajwa .

“Urasimishaji unachukua siku 14 tu, tunakupima kwenye eneo lako la umahiri na tutatathmini na kuangalia maeneo yenye mapungufu na kukujengea uwezo kwenye maeneo hayo na unatoka ukiwa na ujuzi na cheti kinachotambulika,”alisema Rhoda.

Alisema ujuzi ni maisha unapaswa kuwa kwa kila mtu kwa sababu haubagui umri na hauhitaji kuingia gharama kubwa kuupata na kuwa mtu mwenye ujuzi akiutumia anaongeza kipato na kuinua uchumi kwa watu wote awe ameajiriwa au kujiajiri.

Afisa Uhusiano na Masoko wa VETA, David Edward alisema mamlaka hiyo ina jumla ya vyuo 80 nchi mzima vinavyotoa mafunzo katika fani tofauti lakini pia serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vingine 65 ambavyo vinajengwa hadi maeneo ya pembezoni.

“Leng oni vijana na Watanzania wanaopata kupata mafunzo ya ufundi wayapate bila kujali eneo waliloko, VETA imesambaa nchi mzima na na tunakamilisha ujenzi wa chuo chetu mkoani Songwe hivyo kufanya mikoa yote nchini kuwa na chuo cha VETA,”alisema David .

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button