Vijana vyuo vikuu wapewa mafunzo uchaguzi mkuu

DAR ES SALAAM: VIJANA kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini wameshauriwa kushiriki kikamilifu mchakato wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu, kwa kuhamasisha amani na kuzuia ushawishi wa maneno yanayopotosha wananchi dhidi ya kushiriki uchaguzi.

Akizungumza leo Septemba 11, 2025 wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Vijana na Wanawake (TAFEYOCO), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Elvis Makumbo, amesema serikali imetenga bajeti kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa sheria, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania mwenye sifa kujitokeza kupiga kura.

“Kuna taarifa zinazozunguka mitandaoni zikihamasisha watu wasishiriki kupiga kura. Hiyo ni ishara ya kukosa uzalendo. Serikali imetenga fedha kwa ajili ya uchaguzi na ni haki ya kisheria kwa kila Mtanzania mwenye sifa kushiriki. Wananchi wanatathmini viongozi kila baada ya miaka mitano, wasiofaa hubadilishwa na waliowatumikia vyema wananchi hupata nafasi ya kuendelea,” amesema Makumbo.

Kwa upande wake, Laizer Justine, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanachama wa TAFEYOCO, alisema vijana wamepewa elimu kubwa ya kusimamia uchaguzi wa mwaka huu na kuahidi kuwa watakuwa mstari wa mbele kulinda maadili ya taifa.

“Natoa wito kwa vijana wenzangu na Watanzania wote kuunga mkono serikali katika kuratibu jitihada za uchaguzi. Tusiwe watu wa kuiga kauli za kupinga uchaguzi, bali tuhamasishe uchaguzi wa uhuru na amani,” amesema Justine.

Aidha, Kelvin Ernest, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine na mwanachama wa TAFEYOCO, amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa nguzo ya kudumisha amani nchini.

“Tangu enzi za waasisi wa taifa hili, vijana wamekuwa mstari wa mbele kuimarisha uzalendo. Hivyo nasi tunapaswa kufuata mfano huo kwa kuhakikisha amani inaendelea kudumu,” amesema Ernest.

Naye, Maria Marwa, mhitimu wa Chuo cha Takwimu na mwanachama wa TAFEYOCO, amesema vijana wanapaswa kupunguza mihemko na kutumia ushawishi wao kuhamasisha jamii kushiriki uchaguzi kwa amani.

“Sisi kama vijana ni chachu ya kuleta mshikamano na upendo. Hatutakiwi kuwa chanzo cha machafuko, bali tuwe mstari wa mbele kuelimisha jamii yetu kushiriki uchaguzi,” amesema Marwa.

Mkutano huo uliwaleta pamoja vijana wa vyuo vikuu kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujengewa uwezo katika kusimamia uchaguzi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button