Viongozi mitaa watakiwa kutoa elimu ya mazingira

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amewataka viongozi wa serikali za mitaa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa ardhi na uhifadhi wa mikoko katika wilaya hiyo ili kuwa na mazingira bora.
DC Mtambule ameeleza hayo leo jijini Dar es Salaam eneo la Kilongawima katika wilaya hiyo wakati wakipanda miti ya mikoko ambapo leo ni maadhimisho ya mikoko kitaifa huku kidunia huadhimishwa kila tarehe 26 kila mwaka huku akiosema wamepanda miche 1,000 katika eneo hilo.
Aidha, Mtambule amesema asilimia 15 ya watu wa wilaya hiyo wanajihusisha na shughuli katika maeneo ya bahari hivyo ajira zinatengenezwa ,mapato lishe na afya bora hivyo viongozi wa serikali za mitaa wachukulie hatua kali wale wote wanaharibu mikoko katika eneo hilo.
Naye Seleboni Mushi Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Misitu Wizara ya Misitu na Utalii amesema maadhimisho ya mikoko inaangazia mchango mkubwa wa mikoko katika maisha ya wanadamu na ustawi wa ekolojia hivyo husaidia jamii za pwani kuhifadhi fukwe na kuwapatia wananchi kipato pamoja na kuhifadhi chakula kwani inahifadhi hewa ya Kaboni.
Mushi amesema changamoto inayoikabili ni pamoja na uvamizi pamoja na kutoweka kwake tafiti zinaonesha takribani miaka 40 inaonesha nusu ya mikoko duniani inatoweka hivyo kuwa tishio kwa athari za kiuchumi pamoja na hifadhi ya chakula.