Viongozi mitaa watakiwa kuweka pembeni tofauti zao

WENYEVITI na wajumbe wote wa Serikali Za Mitaa wametakiwa kuweka tofauti zao za kisiasa pembeni na badala yake wahamasishe na kuelimisha umma kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Akitoa rai hiyo leo mkoani Mtwara, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara,  Mwalimu Hassan Nyange amesema, nafasi ya mtaa, vijiji na vitongoji ni nafasi muhimu kwenye taifa kutokana miradi ya maendeleo inaibuliwa na inatakiwa kusimamiwa.

Hayo yamejiri wakati wa uapisho wa wenyeviti na wajumbe wa Kamati za Mitaa waliochaguliwa na wananchi kwenye uchaguzi wa Serikali Za Mitaa uliofanyika Novemba 27,2024.

Advertisement

Amesema zipo baadhi ya kazi, majukumu zinapaswa kufanywa na uongozi wa mtaa husika na wananchi ila zinafanywa na halmashauri hivyo amewataka kuhakikisha viongozi hao wanakuwa chachu ya kuhamasisha wananchi kujitolea,kufanya kwa ajili ya maendeleo ya mtaa husika.

Baadhi ya wenyeviti waliokula kiapo hicho  kwa ajili ya kuwatumikia wananchi ikiwemo Mwenyekiti wa mtaa wa Liyawile kata ya Tandika Thomas Chonde amesema atahakikisha anatekeleza ahadi zote alizoahidi kwenye sera zake kipindi cha kampeni ikiwemo kuweka mifereji na kutia kifusi kwenye barabara zote korofi zilzopo mtaani humo.

Mwenyekiti wa mtaa wa Maduka Makubwa Zuwena Njelu amesema :Nitahakikisha anakaa kikao na wajumbe chenye ajenda ya kujenga ofisi ya mtaa ambayo itajengwa kwa muda mfupi.

Aidha, vyama 11  vimeshiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo jumla ya nafasi 666 zilikuwa zinagombewa na nafasi za wenyeviti ni 111 ambazo zote wamechukua chama cha CCM.

Hata hivyo, nafasi ya kundi mchanganyiko 333 zote wakichukua CCM na kundi la wanawake nafasi 221 wamechukua CCM huku nafasi 1 ikichukuliwa na CUF.