Vodacom inavyochochea mageuzi ya kidijitali kupitia ukuaji, matumizi ya data

Dar es Salaam: Vodacom Tanzania imeripoti ongezeko kubwa la matumizi ya data katika mtandao wake kwa mwaka wa fedha ulioishia Machi 31, 2025. Mwelekeo huu umechochea sio tu mafanikio ya kibiashara bali pia ajenda pana ya mageuzi ya kidijitali nchini.
Kulingana na Ripoti ya Mwaka ya 2025, mapato kutoka huduma za data ya simu yalipanda kwa asilimia 21.6 na kufikia TZS bilioni 422.2, huku idadi ya watumiaji wa data ikiongezeka kwa asilimia 19. Idadi ya watumiaji wa simu janja (smartphones) ilipanda kwa asilimia 33.4, na zaidi ya asilimia 70 ya watumiaji wa data sasa wakitumia intaneti kupitia simu janja.
“Ukuaji huu wa matumizi ya data ni kielelezo cha uwekezaji endelevu tunaoufanya katika kupanua na kuboresha mtandao wetu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji, Philip Besiimire. “Kwa kujenga minara mipya 471 ya 4G na zaidi ya asilimia 80 ya matumizi ya data kusafirishwa kupitia 4G, tunawawezesha mamilioni ya Watanzania kupata intaneti ya haraka na ya kuaminika.”
Ongezeko la matumizi ya 4G kwa asilimia 50, kumeimarisha utendaji wa kifedha wa kampuni. Mapato yaliyotokana na huduma yalipanda kwa asilimia 20.5, huku faida baada ya kodi ikipanda kwa asilimia 69.4 na kufikia TZS bilioni 90.5. Mafanikio haya yametokana na kampeni za Vodacom katika kuongeza upatikanaji wa simu janja, na mikopo ya vifaa kwa maeneo ya mjini na vijijini.
Upanuzi wa miundombinu ya Vodacom pia unaendana na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali 2023–2033, unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kidijitali, kukuza ushirikishwaji na kuchochea ubunifu. Kupitia ushirikiano na Mfuko wa Huduma za Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Vodacom imejenga minara mipya 126 ya 4G katika maeneo ambayo hayajafikiwa kwa asilimia zote, hatua inayosaidia kupunguza pengo la kidijitali.
SOMA: Vodacom, Sanlam zaja na mpango wa kuwekeza kidijitali
Zaidi ya hapo, ongezeko la matumizi ya data na simu janja linaunga mkono moja kwa moja malengo ya kitaifa yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayotilia mkazo jamii iliyo na ujuzi wa kidijitali na uchumi wa maarifa. Kwa kupanua huduma za 4G vijijini na kuwezesha upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu kupitia mikopo, Vodacom inachochea ushirikishwaji wa kidijitali na kupunguza pengo la mawasiliano.
“Data ni kama umeme mpya. unaochochea elimu, biashara, afya, utawala, na ujumuishwaji wa kifedha,” alisema Besiimire. “Kwa kuongeza upatikanaji wa simu janja na usambazaji wa intaneti ya kasi hadi vijijini, tunakua kibiashara lakini pia tunaunda jukwaa la maendeleo ya taifa.”
Pata taarifa zaidi kupitia Ripoti ya Mwaka 2025 kupitia: https://www.vodacom.co.tz/financials
Msukumo huu wa kidijitali pia unazisaidia biashara kuwa na wepesi na ushindani zaidi. Kupitia kitengo chake cha biashara, Vodacom inatoa huduma za cloud, intaneti ya kudumu, suluhisho za IoT, na vifurushi vya data kwa biashara, vinavyowawezesha mashirika makubwa na SME kustawi katika mazingira yaliyounganishwa.
“Biashara yetu imekua kwa kasi mwaka huu kutokana na mahitaji makubwa ya huduma za intaneti isiyotumia waya na bidhaa za kidijitali zilizolengwa,” aliongeza Besiimire. “Tunashuhudia mwitikio mkubwa hasa kutoka sekta za elimu, afya, biashara na kilimo.”
Taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Juni imeonesha kuwa Vodacom ina nafasi kubwa zaidi kama mshirika wa pili kwa wingi wa watumiaji wa intaneti isiyotumia waya (fixed wireless), ikiwa na zaidi ya wateja 67,000.
Kadri matumizi ya data yanavyozidi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Mtanzania – kuanzia kutazama video kwenye simu, kujifunza mtandaoni, kufanya biashara hadi huduma za kifedha kidijitali – ni dhahiri kuwa uongozi wa Vodacom katika sekta hii unaendelea kuwa sio tu faida kibiashara bali pia rasilimali ya kitaifa.
Kwa mtazamo wa Dira ya 2030, Vodacom Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kuchukua nafasi kubwa zaidi katika kuunda taifa lenye ujuzi na mawasiliano ya kisasa.



