Vyama, wagombea wapewa masharti kampeni Uchaguzi Mkuu

DODOMA: WAGOMBEA urais, ubunge na udiwani wa vyama 18 vya siasa wanatarajiwa kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu kesho.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatarajiwa kuteua wagombea wa nafasi ya urais, wabunge na madiwani. Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kampeni za uchaguzi zinatarajiwa kuanza kesho hadi Oktoba 28, mwaka huu kwa Tanzania Bara.

INEC imetangaza kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar zitaanza kesho hadi Oktoba 27, mwaka huu ili kupisha kura ya mapema na Oktoba 29, mwaka huu itakuwa siku ya kupiga kura. Vyama 18 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, serikali na INEC wamesaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.

Kanuni hizo zimetengenezwa kwa kuzingatia kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya mwaka 2024. Kanuni hizo zinaweka msingi wa kuzingatiwa na washiriki wa uchaguzi na hatua za kinidhamu zinazoweza kuchukuliwa kwa atakayekiuka vikiwemo vyama vya siasa, wagombea, INEC na serikali.

Kila mgombea, kabla ya kuteuliwa na INEC alitakiwa kuthibitisha kuheshimu na kutekeleza kanuni hizo kwa kujaza na kusaini Fomu Namba 10 mbele ya mkurugenzi wa uchaguzi, msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwa kuzingatia nafasi anayogombea.

Kanuni hizo zinataka vyama vya siasa na wagombea wasifanye fujo au kuchochea vurugu ya aina yoyote katika mikutano ya vyama vingine vya siasa. Vyama na wagombea pia wamezuiwa kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjifu wa amani au kuashiria ubaguzi wa kijinsia, ulemavu, rangi au maumbile kwenye mikutano na kwenye shughuli zote za kampeni.

Kanuni zinataka vyama na wagombea wasifanye kitendo chochote cha unyanyasaji au ukatili wa kijinsia kwa mgombea kinyume na masharti ya Kifungu cha 135 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya Mwaka 2024.

Pia kanuni zinazuia kuruhusu viongozi, wagombea, wanachama na wafuasi wao kubeba silaha yoyote zikiwemo za jadi au zana yoyote inayoweza kumdhuru mtu katika mikutano na shughuli zote za kampeni au mkusanyiko wowote wa kisiasa.

Vyama na wagombea wamezuiwa kufanya au kuruhusu wafuasi na wanachama wao kufanya kampeni kwenye majengo ya ibada na kuwatumia viongozi wa dini kufanya kampeni. Kanuni zinazuia vyama na wagombea kubandua, kuharibu au kuchafua matangazo ya kampeni ya vyama vingine vya siasa na matangazo ya uchaguzi yanayotolewa na INEC au kutumia viongozi, wanachama au wafuasi wao kufanya hivyo.

Pia zinazuia vyama na wagombea kuomba kupigiwa kura kwa misingi ya udini, ukabila au mahali mtu anapotoka, jinsi au rangi na pia wasizuie watu kuhudhuria mikutano ya kampeni ya vyama vingine vya siasa au kutumia wanachama au wafuasi wao kufanya hivyo.

Kanuni zinazuia vyama na wagombea kutumia mitandao ya kijamii kufanya kampeni za chuki, uchochezi, udhalilishaji au ubaguzi wa kijinsia. SOMA: CCM yaahidi kufanya makubwa

Vyama na wagombea wanapaswa kuhakikisha kampeni zinazofanyika ama na wao wenyewe au kupitia wafuasi na wanachama wao kwa zinazingatia misingi inayolenga kutangaza sera zao na zisijenge chuki na mifarakano miongoni mwa wananchi, viongozi na serikali.

Kanuni zinawataka wadau hao wahakikishe mikutano ya kampeni inazingatia ratiba rasmi iliyoratibiwa na INEC, wasimamizi wa uchaguzi au wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika kutangaza sera zao. Vyama na wagombea wanatakiwa kuzingatia muda wa kuanza na kumalizika kwa kampeni na mikutano yote itafanyika kati ya saa 2:00 asubuhi na saa 12:00 jioni.

Pia kanuni zinawataka wadau hao wahakikishe misafara ya kampeni ya chama kimoja cha siasa haikutani na misafara ya kampeni ya chama kingine cha siasa. Kanuni zinawataka wawakataze wanachama au wafuasi wao kutamka kaulimbiu, kuonesha ishara ya vyama vyao vya siasa au kuvaa sare zenye rangi ya chama chao cha siasa katika mikutano ya hadhara ya vyama vingine vya siasa.

Vyama na wagombea wanatakiwa kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuwa lugha itakayotumika katika kampeni za uchaguzi. “Iwapo lugha hiyo haieleweki na itakapolazimu, mgombea atazungumza katika lugha ya Kiswahili na mkalimani atatafsiri katika lugha inayoeleweka kwa jamii husika,” zimeeleza kanuni hizo.

Vyama na wagombea wanatakiwa kuhakikisha wanatumi vijitabu, vipeperushi, vitini, mabango na machapisho ya aina yoyote baada ya kuidhinishwa na INEC kwa upande wa uchaguzi wa rais na msimamizi wa uchaguzi kwa upande wa uchaguzi wa wabunge na madiwani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button