Waandishi watakiwa umakini habari za uchaguzi

DAR ES SALAAM; WAANDISHI wa habari wametakiwa kuwa makini namna wanavyoripoti habari za uchaguzi, hasa zama hizi za teknolojia ya Akili Mnemba (AI).
Wito huo umetolewa katika warsha iliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa kushirikiana na mpango wa #defyhatenow kupitia Global Action for Peacebuilding (GAPI) kwa ufadhili wa GIZ.
Akizungumza katika warsha hiyo, Njokii Kariuki kutoka taasisi ya Global Peace Initiative ya Kenya, alieleza kuwa baadhi ya taarifa huundwa kwa makusudi ili kuchochea hisia, kuharibu sifa za watu au taasisi, hasa katika kipindi nyeti cha uchaguzi.
“Kuna maneno yanaandikwa kwa makusudi ya kuleta taharuki au kuchochea chuki. Waandishi wanapaswa kuwa waangalifu, kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuchapisha taarifa yoyote. Waulize: nani alisema? Lini? Kwa muktadha upi? Na kwa lengo gani?” Amesisitiza Kariuki.

Ameongeza kuwa taarifa nyingi potofu huwasilishwa kwa kutumia muktadha wa zamani, lakini huonekana kama habari za sasa, hali inayoweza kuchangia migawanyiko ya kijamii na vurugu.
Kwa upande wake, Silvia Daulinge kutoka TAMWA amesema kuwa waandishi wanakabiliwa na changamoto kubwa katika ulimwengu wa kidijitali , ambapo taarifa zisizo sahihi husambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii na hata kwenye vyombo rasmi vya habari.
“Kumekuwa na ongezeko la hotuba za chuki na udhalilishaji, hasa dhidi ya wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi. Wanawake, vijana na makundi maalumu wana haki ya kushiriki kikamilifu bila kuonewa au kudhalilishwa,” amesema.

Silvia alisisitiza kuwa mitandao ya kijamii imefungua milango kwa kila mmoja kutoa maoni, lakini ni wajibu wa waandishi wa habari kuchambua kwa makini taarifa hizo na kuziwasilisha kwa njia inayojenga amani, si kubomoa.
“Teknolojia ya akili bandia imerahisisha utengenezaji wa picha, sauti na video bandia zinazoweza kuaminika kuwa halisi. Waandishi wanahitaji maarifa mapya ya kutambua uhalisia wa taarifa hizo,” ameongeza.

Florence Majani kutoka TAMWA naye aliwahimiza waandishi kutumia taaluma yao kama chombo cha kujenga, si cha kubomoa.
“Tunawashauri waandishi kuwa sehemu ya suluhisho. Watumie kalamu zao kujenga jamii yenye mshikamano, kuheshimu haki na usawa, na kulinda misingi ya demokrasia,” amesema.



