Waasi wa ADF wauwa zaidi ya watu 40

KINSHASA: ZAIDI ya watu 40 wameuawa kufuatia mashambulizi ya waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa mujibu wa Jeshi la Congo na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa,waasi hao walishambulia Kanisa Katoliki katika mji wa Komanda, ambako waumini walikuwa wamekusanyika kwa ibada ambapo watu 43 walishambuliwa na kupoteza maisha wakiwemo watoto tisa.
Naibu Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Vivian van de Perre, amelaani mashambulizi hayo na kuyaita uvunjaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu. Mara ya mwisho kwa ADF kufanya mashambulizi makubwa kama haya ilikuwa Februari mwaka huu, ambapo watu 23 waliuawa katika jimbo la Mambasa.
Licha ya operesheni za kijeshi za pamoja kati ya DRC na Uganda, kundi hilo limeendelea kufanya mashambulizi makubwa katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.SOMA : Rwanda, DRC simamieni mkataba wa Washington kudumisha amani



