Wabunge kupiga kura kupitisha bajeti ya serikali leo

WABUNGE leo wanatarajiwa kupiga kura kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 inayotajwa ni ya mageuzi ya kiuchumi.
Watapiga kura bungeni Dodoma kwa kuitwa jina ili watamke ndiyo au hapana.
Kwa kuzingatia mabadiliko ya kanuni yaliyofanywa hivi karibuni hata wabunge ambao watakataa kupiga kura kwa kutamka ‘abstain’ uamuzi wao utawekwa kwenye kumbukumbu kuwa wamesema sipigi kura.
Kwa siku saba tangu Juni 16 mwaka huu wabunge walichangia taarifa ya hali ya uchumi, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2025/2026 na mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Juni 12 mwaka huu Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti ya serikali ya Sh trilioni 56.49 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kwa kuzingatia waliyosema wabunge wakati wakichangia mapendekezo hayo bajeti hiyo inatarajiwa kupitishwa kwa kishindo bungeni jijini Dodoma.
Wakati wakichangia mapendekezo hayo, wabunge waliishukuru serikali kwa kupeleka fedha nyingi za kutekeleza miradi kwenye majimbo yao na wengi wao wakasema hawana cha kumdai Rais Samia Suluhu Hassan.
Waliipongeza serikali kwa kuweka mikakati ya kutafuta vyanzo vya mapato kugharamia programu za afya ya wananchi zikiwemo za Ukimwi na Bima ya Afya kwa Wote.
Wabunge waliipongeza serikali kuwezesha wananchi kiuchumi na wameishauri itekeleze mikakati kuongeza idadi ya walipakodi.
Walishauri serikali iboreshe mazingira ya biashara kuongeza fursa za ajira na iimarishe mifumo ya kukusanya mapato kuongeza makusanyo.
Imeshauriwa iongeze umakini kufuatilia ukweli kuhusu viwango vya hisa kwenye miradi ya uwekezaji inayotekelezwa kwa ushirikiano wa wageni na wazawa ili nchi inufaike.
Pia wabunge walisifu hali ya utulivu wa nchi na mwelekeo wa bajeti kuthamini maisha ya Watanzania.
Bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2025/2026 ni ya tano na ya mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26).
Bajeti hiyo inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani ya Sh trilioni 40.47, misaada Sh trilioni 1.07 na mikopo ya Sh trilioni 14.95.
Kati ya mapato ya ndani yanayotarajiwa, mapato ya kodi ni Sh trilioni 32.31, mapato yasiyo ya kodi Sh trilioni 6.48 na mapato ya mamlaka za serikali za mitaa Sh trilioni 1.68.
Aidha mikopo inajumuisha Sh trilioni 6.27 kutoka vyanzo vya ndani na Sh trilioni 8.68 kutoka vyanzo vya nje.
Wakati akiwasilisha mapendekezo ya serikali bungeni Juni 12 mwaka huu, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema dhima kuu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ni mageuzi jumuishi ya uchumi kupitia uimarishaji wa ukusanyaji mapato ya ndani, uwekezaji wa kimkakati wenye kuzalisha fursa za ajira na uboreshaji wa hali ya maisha ya wananchi.
Katika mwaka wa fedha 2025/2026 serikali ina lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2025 kutoka ukuaji wa asilimia 5.5 mwaka 2024.
Serikali pia inataka mapato ya ndani yafikie asilimia 16.7 ya Pato la Taifa mwaka 2025/2026 ikilinganishwa na asilimia 15.8 mwaka 2024/2025 na mapato ya kodi yafikie asilimia 13.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025/2026 kutoka asilimia 12.8 mwaka 2024/2025.