Wabunge sasa kutoa ahadi ya uadilifu

ODOMA; BUNGE leo limepitisha mapendekezo ya maboresho ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ambapo miongoni mwa maboresho hayo ni wabunge kutoa ahadi ya uadilifu katika kila kikao cha kwanza cha Mkutano wa Bunge.

Mapema leo asubuhi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge, Mussa Azzan. aliwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu Marekebisho au mabadiliko katika Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023.

“Mheshimiwa Spika, baadhi ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola yanao utaratibu wa Wabunge kutoa ahadi ya uzalendo katika vikao vyake.

“Hivyo, inapendekezwa tuweke utaratibu huo katika Kanuni ambapo Wabunge watatoa ahadi ya uadilifu katika kila Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Bunge, ambapo kila Mbunge ataahidi kuwa mtiifu na mwaminifu kwa nchi yetu na kufanya kazi zake kwa uadilifu.

“Aidha, uzoefu wa nchi nyingine za Jumuiya ya Madola, unaonesha kuwa Wabunge hutoa ahadi kwa nchi na wananchi wake. Ahadi hii hutolewa kabla ya kuanza vikao vya Bunge. Ahadi hiyo humaanisha kuwa, wabunge watakuwa wazalendo wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kibunge.

“ Kwa kuwa utaratibu huu haupo katika Bunge letu, Kamati inaona kuwa ni muhimu kuiga utaratibu huu mzuri,” amesema Makamu Mwenyekiti. Bunge kwa kauli moja limeazimia kupitisha maboresho ya kanuni hizo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button