Wachepusha maji Mto Malagarasi kuzalisha umeme

KIGOMA; Kampuni ya DongFang Electric (DEC) imefanikiwa kuchepusha maji ya Mto Malagarasi katika eneo la Igamba, Kijiji cha Mwamila Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ili kuanza ujenzi wa tuta la bwawa la kuzalisha umeme kutoka Mto Malagarasi.

Tukio la kufunga rasmi njia ya awali ya mto huo na kuelekeza katika njia nyingine limeshuhudiwa na Mkurugenzi wa Kanda ya Magharibi wa Shirika la uzalishaji na usambazaji umeme nchini (TANESCO), Richard Swai kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Razalo Twange.

Akieleza kutekelezwa kwa uchepushaji huo, Kaimu Mhandisi Mkazi wa kampuni ya DEC, Han Wel amesema mpango huo wa kuchepusha mto ulipaswa ukamilike Agosti 27, mwaka huu lakini wamekamilisha jambo hilo siku 10 kabla ya muda wake ili kuwezesha kuanza ujenzi wa tuta la kukusanyia maji (Bwawa) ikiwa ni sehemu ya kuanza mradi wa ujenzi wa mradi huo.

AkizungumzaMkurugenzi wa Kanda ya Magharibi wa shirika hilo, Richard Swai, alisema kuwa uchepushaji huo wa mto ni hatua ya awali ya kupata sehemu kavu ili kujenga tuta la kupeleka maji kwenye mitambo ya kuzalisha umeme na kwamba hadi sasa mradi umefikia asilimia 10 na upo ndani ya wakati.

Swai alisema kuwa mradi huo utakapokamilika mwezi Oktoba mwaka 2027 utawezesha kuzalisha umeme wa megawatt 49.5 na kwamba kitachangia kwa kiasi kikubwa gridi ya taifa sambamba na kuifanya Kanda ya Magharibi kuwa mzalishaji na mchangiaji wa umeme kwenye gridi ya Taifa, jambo ambalo kabla ya hapo halikuwepo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button