MKUU wa Mkoa wa Manyara, Quinee Sendiga amewataka wachimbaji wa madini katika Mkoa wa Manyara kushirikiana katika kufanya kazi za uchimbaji na biashara lengo ni kukuza uchumi wa mkoa huo.
Sendiga amesema hayo mara baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama Cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) na kusema kuwa siri kubwa ya kufanikiwa ni kufanya biashara na uchimbaji kwa kufuata sheria.
Amesema ukifanya biashara kwa njia ya mkato na kutaka kutorosha madini kwa njia ya panya shughuli za uchimbaji na ufanyaji biashara hazitakuwa na maisha marefu kwani dola inaweza kukutia mbaroni na kukumaliza kibiashara.
Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wafanyabiashara wa madini mkoani Manyara kuhakikisha wanakuza uchumi wa Mkoa huo ili uwe na maendeleo ya kutosha tofauti na sasa.
Amesema na kuwataka viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo kuhakikisha wanaongoza MAREMA kwa weledi na mshikamano ili lengo liwe moja kukuza uchumi wa Mkoa wa Manyara kwa faida ya wananchi wote.
‘’Nataka mchague viongozi Bora wenye sifa za kuongoza na sio bora viongozi kwani serikali ya Mkoa wa Manyara inahitaji viongozi bora wenye mtazamo wa maendeleo ya baadae’’alisema Sendiga
Akizungumza baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa MAREMA Mkoa wa Manyara,Elisha Mnyawi amewaomba wachimbaji wote Mkoa wa Manyara kushirikiana,kushikamana na kufanya kazi kwa kufuata sheria zilizowekwa na Wizara ya Madini.
Mnyawi alisema katika uongozi wake atahakikisha anatenda kazi kwa kufuata sheria na kanuni za Wizara ya Madini na kamwe hatamwonea mchimbaji kwa mslahi fulani kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka maadili ya uongozi na hilo katika uongozi wake halitakuwepo kamwe.
Amesema kila siku viongozi wa serikali wanasisitiza wafanyabiashara wa madini kufanya biashara ya madini kwa kufuata sheria ikiwa ni pamoja na kulipa kodi halali ya serikali hivyo yeye atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha hilo analisimamia kwa asilimia kubwa ili kila anayestahili kulipa kodi analipa ili pande zote ziweze kufaidi.
Wengine waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni pamoja na nafasi ya Makamu Mwenyekiti amechaguliwa Money Yousuph, Katibu Mkuu wa Marema amechaguliwa Tariq James,Katibu Msaidizi amechaguliwa Dk Curtyus Msosa, Nene Lyimo amechaguliwa kuwa mtunza hazina, mhazini msaidizi amechaguliwa Samweli Lugemalila na Joseph Manga amechaguliwa kuwa mjumbe kamati ya nidhamu na usuluhisho.
Wengine waliochaguliwa kuongoza Marema Mkoa wa Manyara ni pamoja na Rachael Njau mjumbe upande wa wanawake,Antony Mavili mjumbe wasio rasmi na Regan Kafuruki amechaguliwa kuwa mjumbe kupitia vijana.