Wachumi waeleza athari mgogoro wa Israel, Iran

WACHAMBUZI wa masuala ya uchumi wamesema mgogoro kati ya Israel na Iran unaoendelea unaweza kuleta athari za kuongezeka kwa mfumiko wa bei za bidhaa muhimu na mafuta.
Wakizungumza na HabariLEO jana, wachambuzi hao walisema nchi hizo ni moja ya wazalishaji wa mafuta yanayotumika duniani na Tanzania ni moja ya waagizaji wa bidhaa hiyo.
Mtaalamu wa uchumi, Walter Nguma alisema makombora yanayoendelea kurushwa yanaharibu miundombinu ya usafiri, hivyo kupunguza uzalishaji wa mafuta na matokeo yake ni kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa bidhaa nchini.
Nguma alisema kwa sasa athari hazitaonekana mapema kwa sababu nchi inatumia akiba ya mafuta iliyopo, lakini uagizaji unaokuja utakutana na changamoto ya bei kuongezeka.
Alisema athari nyingine ni kupungua kwa mzunguko wa biashara na masoko ya kimataifa kwani wakati huo wa mgogoro baina ya nchi hizo biashara itakuwa ndogo.
Aliishauri serikali kuimarisha sera zake za mambo ya nje na kuimarisha uzalishaji wa ndani na kuweka mikakati ya kuinua masoko ya ndani ya nchi ili kuweka utegemezi.
Meneja wa Masuala ya Ushuru na Ushirika kutoka Mgodi wa AngloGold Ashanti ambaye ni mchumi, Godvictor Lyimo alishauri serikali kuweka vivutio vya kikodi kwenye gesi asilia ili kupunguza utegemezi katika matumizi ya mafuta kwenye viwanda na vyombo vya usafiri.
Lyimo alisema ni muhimu kwa wananchi kugeukia matumizi ya gesi asilia katika maeneo ya viwanda, uzalishaji umeme na magari.
“Wananchi watambue bei za mafuta zitapanda, kwa hiyo wabadilike na wabadilishe mifumo ya mafuta kwenye magari yao waende kwenye matumizi ya gesi asilia ambayo tunayo nchini,” alisema Lyimo.



