Wadau wa malezi wanolewa Mtwara

WADAU kutoka Asasi mbalimbali za kiraia zinazojishughulisha na masuala ya watoto kuanzia mwaka 0 mpaka 8 mkoani mtwara wamenolewa kwa kupatiwa elimu kuhusu Mtandano wa Malezi na Makuzi ya Watoto Nchini (TECDEN).
Akizungumza wakati wa mfunzo hayo Meneja Miradi kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Kitovu cha Maendeleo Safi la KIMAS mkoani Mtwara, Torai Kibiti amesema wameona ipo haja ya kuwapatia elimu hiyo wadau hao ambao kwa namna moja ama nyingine walikuwa hawajui uwepo wa mtandao huo.

Amesema Shirika la KIMAS linafanya kazi kwa kushirikiana na TECDEN pamoja na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara hivyo wametoa elimu kwa wadau hao ili waweze kufahamu kazi na majukumu yanayofanywa na mtandao huo wa malezi na makuzi ya watoto nchini .
Hata hivyo wametoa ufahamu au uelewa kwa wadau hao kuhusu Program jumuishi ya Taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM) inayolenga kuleta uratibu wa masuala ya watoto kuanzia mwaka 0 mpaka 8.
‘’Serikali ilifanya utafiti na kugundua kwamba shughuli zinazohusu watoto kuanzia mwaka 0 mpaka 8 zinafanyika lakini kila mdau anafanya kwa namna yake hivyo serikali ikaja na program hii ambayo sasa inalenga kuleta uratibu mzuri kwamba kila sekta, mdau anayehusika afanye kwa kushikiana’’amesema Kibiti.

Kwa upande wake Mwandishi Kinara na Mkufunzi wa Habari za Watoto kutoka PJT-MMMAM, Gregory Millanzi amesema katika umri huo mwaka 0 mpaka 8 ukuaji na ujifunzaji wa watoto huanza matokeo kupitia milango yao ya fahamu ikiwemo kusikia, kunusa.
Hata hivyo kuona, kuonja na mengine lakini pia watoto hao wanajifunza kupitia kucheza huku akiwaomba wazazi mkoani humo kuwa karibu na watoto ili waweze kukua vizuri kwenye ubongo wao.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Mtwara, Anna Sallu amesema kwenye eneo hilo la malezi wamewaita wadau hao ili waweze kuwasaidia kutoa elimu juu ya ushiriki wa wazazi hasa wa kiume.
‘’Tumeona kuwa programu hii inahitaji wazazi washirikiane kwenye malezi ya mtoto tangu anapokuwa na umri wa mwaka 0 anapokuwa tumboni, anapozaliwa mpaka anapofikisha umri wa miaka 8’’amesema Sallu
Aidha program hiyo ni ya miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2026 ambayo ndani yake inaratibu kwenye upatikanaji wa huduma bora kwenye maeneo matano ikiwemo lishe bora, afya, ulinzi na usalama, fursa za ujifunzaji za awali na malezi yenye mwitikio.



