Wadau wa mazingira wafanya usafi Mwanza

MWANZA: Wadau wa mazingira wamefanya usafi katikati ya jiji la Mwanza na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira, ili pamoja na mambo mengine, kuzuia magonjwa ya mlipuko.

Hatu hiyo ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani leo Septemba 20, 2025, Ofisa Mazingira Mwandamizi wa Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene, amesema aina mojawapo ya taka zinazoathiri mazingira ni zile zenye asili ya plastiki, na idadi yake inakua kadri siku zinavyonga kiasi kwamba zisipodhibitiwa zinaweza kuchukua eneo kubwa kuliko hata la binadamu.

“Taka hizi zinaharibu pia vyanzo vya maji na kuathiri viumbe hai waliomo. Hii ni kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanyika katika pande mbalimbali za dunia.

“Zinaonesha kukithiri kwa taka hizi katika baadhi ya vyanzo vya maji duniani, ikiwemo Ziwa Victoria, kiasi cha kuelekea hata kuzidi idadi ya samaki,” amesema.

Kwa jiji la Mwanza, amesema taka nyingi zinatupwa katika mitaro, kisha kusombwa na maji kipindi cha mvua kuelekea Ziwani, hatimaye kuathiri samaki.

Ofisa Mazingira wa taasisi isiyo ya kiserikali EMEDO, Kitongo Lawrence, amewaelimisha wananchi kwamba suala la kutunza mazingira ni la kila mwanajamii, na si la serikali na washirika wake tu.

“Hivyo kila mwananchi anapaswa kuwa kiongozi wa mazingira yanayo mzunguka,” amesema.

Balozi wa Mazingira kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Mrisho Mabanzo, maarufu kama ‘Mr Tree’, amesema, pamoja na mambo mengine, anaendesha kampeini ya ‘Ziwa Letu Festival’ inayolenga kutunza Ziwa Victoria kwa kulifanyia usafi mara kwa mara ndani na kandokando.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button