Wadau waiomba CBT kuboresha takwimu za wakulima

WADAU mbalimbali wa zao la korosho wameiomba Bodi ya Korosho Tanzanzani (CBT) kuendelea kuboresha zoezi la uhaulishaji wa kanzidata za wakulima wa zao hilo ili kupata takwimu halisi za wakulima wa zao hilo.

Akizungumza leo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara (RCC) mwaka 2024 kilichofanyika Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba Baisa Baisa amesema suala linalokwamisha ufanisi wa zoezi hilo ikiwa ni pamoja na usimamizi wa maslahi ya watendaji wa kazi hiyo.

Advertisement

Ameishauri Cbt kuendelea kuboresha usimamizi wa zoezi hilo la usajili ili liweze kufanyika vizuri na kwa ufanisi mkubwa na kuondokana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima kuhusu kutofanya vizuri kwa mfumo huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Yusuph Kateule “Niwaombe bodi kwenye vijiji vijana wenyeji wapo wana elimu na uwezo wa kufanya kazi, wana vitendea na kazi itakuwa mzuri”

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa CBT, Mangile Malegesi amesema msimu ujao wa korosho mwaka 2025/2026 watahakikisha miongoni mwa changamoto zilizojitokeza msimu uliyopita mwaka 2023/2024 hazijitokeza tena ikiwemo watoto wadogo kujitokeza kwenye mfumo huo kwa madai kuwa ni wakulima wa korosho.

“Msimu wa korosho uliyopita 2023/2024 vijana tuliyokuwa tunawatumia katika zoezi hili kuna wakati walikuwa wanaingiza takwimu za wakulima zisizokuwa sahihi”

“Sisi bodi ya korosho tumeshaajiri vijana mia tano ambao siyo ajira rasmi ambao tutawagawa kwenye kila kijiji kinacholima korosho ili wafanye kazi za kuhuisha taarifa za wakulima na tutaanza kuwapa mafunzo kuanzia Januari 2, hadi Januari 10, 2025 baada ya hapo tuwagawe kwenye vijiji vyote,”amesema Malegesi.

Hata hivyo vijana hao hawataishia katika zoezi hilo la kuhuisha kanzidata za wakulima bali watasimamia pia usambazaji wa pembejeo za korosho, kutoa elimu kwa wakulima ikiwemo kuwapatia ushauri wa namna ya kutunza mikorosho yao.

Pia kufufua mashamba pori, kuondoa mikorosho yote ile isiyoweza kuzaa lakini ukifika msimu huo wa korosho mwaka 2025/2026 watahakikisha wanasimamia wakulima waweze watunza vizuri korosho zao kabla ya kuzipeka kwenye chama cha msingi(AMCOS).

Aidha zoezi hilo la usajili wa wakulima hao kwa njia ya mfumo lilianza rasmi katika msimu wa kilimo mwaka 2022/2023 kwani lengo la serikali ni kuhakikisha inapata idadi kamili ya wakulima wa zao hilo ili inapogawa pembejeo za korosho igawe kulingane na idadi kamili ya mikorosho.

Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala ametoa wito kwa viongozi na wadau wa mnyororo mzima wa korosho kuendelea kudhiti na kusimamia zao hilo ili liendelee kufanya vizuri.