Wadau wajadili umeme nishati salama

Tanzania ikiwa inafungua mkutano wa masuala ya nishati unaokutanisha wakuu wa nchi za Afrika kesho, wadau mbalimbali wa nishati safi nchini wamekutana mwishoni mwa wiki iliyopita kujadili njia mbadala za upatikanaji wa umeme kupitia nishati salama.

Mkutano huo uliondaliwa na kampuni ya Clarke Energy Tanzania inayojishughulisha na usimikaji wa mitambo ya umeme wa gesi asilia, ulilenga kuwakutanisha wadau hao kujadili njia mbadala za upatikanaji wa umeme wa uhakika lakini pia kuwa na matumizi ya nishati rafiki wa mazingira.

Naibu Meneja Mkuu wa Clarke Energy, Tarak Jani, amesema kukatika kwa umeme mara kwa mara kunapunguza uwezo wa viwanda kuzalisha bidhaa zinazoendana na hali ya uchumi wa Watanzania lakini pia inaathiri uchumi wa nchi hivyo kuna umuhimu wa wadau kukaa pamoja kutafuta mbadala.

Amesema ushirikishwaji wa wadau katika uzalishaji wa nishati safi unatajwa kuwa suluhu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika na kumaliza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Naibu Meneja Mkuu wa Clarke Energy, Tarak Jani akizungumza na wadau kwenye mkutano huo.

Amesisitiza ushirikiano wa serikali na wadau katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa kuwa changamoto iliyopo kwa sasa Tanzania si uzalishaji wa umeme bali usambazaji wa uhakika wa nishati hiyo.

Ameeleza kuwa Clarke Energy imesaidia ukuaji wa uzalishaji viwandani kwa kutoa mitambo yenye mifumo ya hali ya juu na huduma za msaada wa kiufundi ili kuimarisha mifumo ya nishati nchini.

“Kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Clarke Energy tunatoa mitambo ya kuzalisha umeme inayotumia gesi asilia ili kutoa ufumbuzi wa nishati safi viwandani, ambayo ni rafiki wa mazingira ikilinganishwa na dizeli, makaa ya mawe na nyinginezo,” alisema.

Aidha Jani amesema kuwa mbali na huduma wanazotoa, kampuni hiyo pia inatoa mafunzo kwa wateja wake juu ya kutumia kwa ufanisi mitambo ya kuzalisha umeme wa gesi asilia katika namna ambayo itapunguza uzalishaji wa hewa ukaa ambayo ni hatari kwa mazingira kwani inachangia ongezeko la joto duniani.

“Tunalenga kuchukua hatua madhubuti za kuboresha sekta ya nishati nchini Tanzania kwa kushirikiana na mashirika muhimu kama TANESCO na TPDC ili kuhakikisha umeme wa uhakika kwa viwanda, taasisi na jamii,” alisema.

Naye Meneja Mkuu wa Clarke Energy, Emile Hamman, amesema kuwa kampuni hiyo inaweka kipaumbele katika kuimarisha sekta ya nishati kupitia ushirikiano na viwanda, wazalishaji huru wa umeme (IPPs), na wakala maalumu wa serikali.

“Clarke Energy haiwekezaji moja kwa moja katika miradi ya kuzalisha nishati, …hutoa vifaa vya kuzalisha umeme na huduma za baada ya mauzo kwa wateja wake. Kwa mfano, kituo cha kuzalisha umeme cha Somanga mkoani Lindi ni moja ya maeneo ambayo tumewezesha uzalishaji wa nishati kwa kutumia gesi asilia,” alisema Hamman.

Mmoja wa wawakilishi kutoka Kampuni ya Lodhia ya Mkuranga mkoani Pwani, ambayo inahudumiwa na mitambo kutoka Clarke Energy amepongeza juhudi za kampuni hiyo katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika viwandani kupitia nishati salama na kuongeza kuwa kiwanda chake kilipokea mtambo unaozalisha megawati 5 za umeme.

Amesema pamoja kutoonesha kuvutiwa na huduma hiyo awali, Clarke Energy hawakukata tamaa kuwaelimisha mpaka pale walipokubali na sasa wamepata suluhu ya kukatika kwa umeme kiwandani kwao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button