Wadau wakumbushwa umuhimu elimu jumuishi

MTWARA: JAMII na wadau mbalimbali wa elimu mkoani Mtwara wamekumbushwa umuhimu wa elimu jumuishi kwa wanafunzi hasa wenye mahitaji maalumu ili wajione nao wanapata haki sawa ya kielimu kama ilivyokuwa wanafunzi wengine.

Hayo yamejiri wakati wa kikao cha wadau wa elimu cha siku moja kuhusu kujadili utekelezaji wa elimu jumuishi, mafanikio, changamoto na kuweka mikakati kupitia mradi wa ‘Sauti Zetu’ unaotekelezwa na Taasisi isiyo ya kiserikali linalojishguhulisha na masuala mbalimbali ya kijamii mkoani Mtwara (MTWANGONET) chini ya Haki Elimu.

Akifungua kikao hicho Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Joel Mkuchika amesema suala la kupata elimu haiwezeshwi tu shuleni bali linaanzia kwenye jamii pamoja na wadau ambapo kila mmoja ana nafasi ya kuwezesha upatikanaji wa elimu hiyo.

Kikao hicho kimekutanisha wadau hao wa elimu kutoka halmashauri ya Wilaya ya Mtwara pamoja na Manispaa ya Mtwara Mikindani na kufanyika kwenye manispaa hiyo.

‘’Kuna nafasi ya mzazi licha ya mwanafunzi, jamii ambayo ndani yake ina makundi mbalimbali, kila watu wana nafasi yao na kila kundi litakaposhiriki kikamilifu katika mchakato wa kuhakikisha kila wanajamii ananufaika na elimu na masuala mengine kwenye jamii ndipo tutaweza kufanikiwa,’’amesisitiza Joel.

Naye Ofisa Elimu Maalumu Sekondari katika manispaa hiyo ,Hilda Hinjo ameyataja makundi ya wanafunzi hao wenye mahitaji maluumu katika elimu jumuishi ikiwemo wenye ualbino, ulemavu wa viungo,wenye usonji, wasioona, viziwi na viziwi wasioona.

Ofisa Ustwai wa Jamii wa Manispaa hiyo, Godlove Miho amesema kwa sasa jamii imehamasika kuhusu kuwapeleka watoto wenye mahitaji shule ambapo kwa mwaka 2025 wamefanikiwa kumpata mtoto mmoja tu kwenye manispaa  aliyefichwa ndani lakini bado wanaendelea kufanya ufatiliaji ili kubaini kama kuna watoto ambao bado wamefichwa.

Mratibu wa Mradi huo wa ‘Sauti Zetu’ kutoka Mtwangonet Deogratius Makoti amesema kikao hicho kimejumuisha makundi yote ya pembezoni kwasababu mradi unalenga kuchochea utekelezaji wa mkakati wa elimu jumuishi wa taifa katika masuala ya jinsia na usawa wa kijinsia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button