Wadau waombwa kusimama na wenye ulemavu

MOROGORO: MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kupitia Dawati la Watetezi la watu wenye Ulemavu ( DDI) umetoa rai kwa watanzania wote , taasisi za kiserikali , asasi za kiraia na wadau wa maendeleo kuungana nao katika kusimamia kidete na kutetea haki za watu wenye ulemavu .

Mkuu wa Dawati la Watetezi la Watu wenye Ulemavu kutoka THRDC ,Mwanasheria Emmanuel Majeshi, amesema hayo kwenye tamko la siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu iliyofanyika kitaifa Desemba 3, 2025 mkoani Morogoro.

Majeshi amesema katika kuadhimisha siku hiyo muhimu mwaka huu, dawati litaendeleza dhamira yake thabiti ya kusimamia , kulinda na kukuza haki pamoja na ustawi wa watu wenye ulemavu nchini.

Hivyo amesema ni wajibu wetu sote kuendelea kuimarisha upazaji wa sauti za watu wenye ulemavu ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kujenga jamii jumuishi, na kuwawajibisha wale wanaokiuka haki zao.

“ Tunaamini kwa dhati kuwa ushiriki na uongozi wa watu wenye ulemavu ni kiini cha kujenga jamii yenye usawa na inayotoa nafasi kwa kila mmoja kuchangia na kustawi bila vizuizi” amesema Majeshi.

Katika hatua nyingine THRDC) kupitia Dawati hilo limetoa wito wa kuwepo kwa mapitio ya mara kwa mara ya Sera, Sheria na Miongozo ambayo itaimarisha na kusaidia ustawi wa watu wenye ulemavu.

Mkuu wa Dawati hilo aemsema kuna umuhimu wa kuwa na mifumo, sera na sheria rafiki ambazo zitazingatia ustawi mkubwa wa jamii ya watu wenye ulemavu.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania ( SHIVYAWATA ) ,Jonas Lubago ameeleza kuwa maadhimisha hayo pia yametumika kuelimisha jamii kuhusu upatikanaji wa haki kwa watu wenye ulemavu ikiwemo maeneo ya kutoa huduma ili kuhakikisha kunakuwepo usawa na huduma zinazowafikia watu wote bila kuacha kundi hilo muhimu.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS) , Abdallah Omari ameiomba Serikali kuandaa mpango mkakati wa kuhakikisha kila sekta kunakuwepo na njia nzuri za kuwaendeleza watu wenye ulemavu.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu mwaka 2025 yamebeba kauli mbiu: ”Kuendeleza jamii jumuishi kwa watu wenye Ulemavu kwa Mstakabali wa Ustawi wa jamii”.

Habari Zifananazo

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button