Waeleza walivyonufaika na mikopo

ARUSHA: WAJASIRIAMALI wawili ni miongoni mwa wanufaika wa mfuko wa SELF Microfinance ambao wamewaomba wajasiriamali wengine kutumia mfuko huo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Wajasiriamali hao wakiongea na wajumbe wa wa Bodi ya SELF Microfinance wameshukuru kutembelewa mkoani Arusha ili kujionea jinsi wanavyonufaika na mikopo nafuu inayotolewa na mfuko huo.
Kwa nyakati tofauti wakizungumza, wajasiriamali hao wamesema hawajawahi kujuta kupata mkopo huo, wamepata manufaa makubwa, biashara zao zimekua kwa kasi na kuinuka kiuchumi.
“Nimeweza kutoka kufuga kuku 400, sasa nina kuku 1,200. Awali nilikuwa naokota mayai ‘trei’ 12 kwa siku sasa hivi naokota ‘trei 30 kwa siku,” amesema Teddy Mtinangi.
Ameieleza bodi hiyo kwamba awali alikuwa anapata faida sh, 900,000 hadi sh, milioni 1lakini baada ya kupata mkopo huo anapata faida sh, milioni3 na soko likichangamka hupata hadi sh, milioni4
Naye, Teddy Mchome mmiliki wa ‘Teddyjoo naturals’ ambao wanatengeneza bidhaa za nywele na ngozi kwa malighafi ya mimea asili amesema SELF Microfinance imempa fursa ya kuongeza mtaji wake.
“Bidhaa zetu hazina viambata sumu, kabla [mkopo] tulianza na wateja wachache kwa sababu tulikuwa hatujapanuka, mtaji ulikuwa mdogo lakini tulikutana na SELF Microfinance walitusaidia,”
Nao wajumbe wa Bodi ya SELF Microfinance wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Paul Sangawe pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Santieli Yona, wamejionea namna wajasiriamali hao walivyoweza kukuza biashara zao.